
Namshukuru Mungu kwa Afya njema na kwa kuniwezesha kufanya
ziara ya kulitembelea jimbo letu la Bukombe. Ziara hii imenichukua siku 20
ambapo nilitembelea kata 16 na kata moja mkutano wetu uliahirishwa kutokana na msiba uliojitokeza eneo tulilopanga mkutano.
Nawashukuru sana wananchi
wenzangu wa kata zote kwa mapokezi mazuri waliyonipatia wakati wa ziara yetu. Nawashukuru pia kwa
vikundi mbalimbali vya sanaa vilivyotumbuiza mikutano yetu, tumbuizo hizo
pamoja kuburudisha mikutano yetu, ziliibua hoja za mjadala; kero mbalimbali zilitolewa
kupitia kazi hizo za sanaa. Vyovyote vile wananchi kwenye kata tulizotembelea walikaa kwetu mikutano toka mwanzo na hata
mwisho wake.
Nawashukuru sana
waheshimiwa Madiwani wetu wa kata zote pamoja na watendaji wetu wa kata na
vijiji vyote tulivyovitembelea kwa kazi njema ya kuandaa mikutano hii tena kwa
taarifa ya muda mfupi.
Nawashukuru pia wataalamu
wote wa idara zote wa ngazi zote kwa kutusaidia sana kufafanua baadhi ya hoja
za wananchi zilizojitokeza wakati wa kipindi cha ziara hii. Majibu yao yalitupa msingi na mwelekeo wa ufahamu. Bila shaka
wasingekua wao, mimi ningekua wa majibu yasiyo na uhakika ama yale yakusema
...”swala hilo nimelichukua ...” lakini walijibu kadri walivyoweza na kwa
kiwango cha kuridhisha.
Mwisho nawashukuru wote
tulioambatana pamoja kwenye ziara yetu Dereva wetu Shija Malembela, katibu wa mbunge ndg Benjamini Mugeta, Ndg Salum
Mkadam Ndg Nelvin Sarabaga. Wote hawa waliifanya ziara yetu iwe rahisi.
YALIYOJTOKEZA
Sikuwahi kufikiri kama wananchi wa Bukombe wana kiu ya maendeleo kwa kiwango kikubwa namna
ile.
Ziara yetu ilikuwa na mahudhurio makubwa ya wananchi,
aidha wananchi kwa wingi
walijitokeza kuulizwa maswali mengi
sana, ( hapa lazima nikiri) wengi walikosa nafasi ya kuuliza kwa sababu ya
muda. Wote waliopata nafasi waliuliza
maswali ya msingi sana kwa manufaa ya wananchi wote bila kujali tofauti zao (za kikabila, dini, upenzi wa vyama vya siasa
n.k.) yaliyojitokeza ni mengi lakini hapa nitaelezea yaliyojitokeza kila mahali
tulipofanya mkutano, kama ifuatavyo:-
1.
MAJI
Wilaya
yetu ya Bukombe ipo nyuma sana kwa miradi ya maji. Miradi ya maji iliyopo
wilayani kwetu ni ule wa kilimahewa, Msasa Runzewe Magharibi visima 8 (kwa
juhudi ya Mhe. Diwani kupitia shirika la RUDDO), Bulega na Mradi wa uyovu.
Mradi
wa Musasa ulishakufa, mradi wa Kilimahewa unafanyakazi chini ya kiwango, miradi
ya uyovu mmoja tu unafanyakazi lakini mmoja wa kwa Mzibila haufanyi kazi kutokana na ubovu wa pump. Bulega
unafanya kazi ila wa Ibambilo haufanyi kazi.
Kwa
kifupi sehemu kubwa ya wilaya yetu haina miradi sehemu nyingi ya maji, wananchi
wanapata maji kutoka kwenye visima vya asili ambavyo haviwahakikishii usalama
wa maji. Utaona ukweli kuwa Bukombe shida ya maji ni kubwa mno kuliko inavyoelezwa.
Wananchi
wanatamani kuona kero hii inapunguzwa kwa haraka. Kazi hii ni ya serikali naamini
kama mwakilishi wa wananchi ni kulisukuma kwa nguvu zote jambo hili ili
tupunguze changamoto hii kubwa.
Kazi
hii nitaianza, kuanzia Bunge la Bajeti lijalo linalotarajiwa kuanza tarehe 17/04/2016.
Nawaomba wananchi wenzangu kuwa na subira wakati nikifatilia jambo hili nyeti
na muhimu.
Aidha
kwenye ngazi ya Halmashauri nawaomba na kuwasihi madiwani tuanze kuibua miradi ya maji kwenye
maeneo yetu. Hii itaisaidia serikali kupunguza gharama za utafiti. Nimeiomba
pia halmashauri kuondoa mazingira yote, ambayo yanapelekea miradi kuwa chini ya kiwango, mwisho wake fedha
zinatumika ila wananchi hawapati maji. Imani yangu serikai nayo itaongeza
msukumo wa kuleta miradi ya maji kwenye wilaya yetu. Katika ziara yetu jumla ya
maswali 305 yaliulizwa mbapo katika hayo maswali 193 yalihusu maji, kutokana na hali hii ni dhahiri suala
la maji linawapa usumbufu mkubwa wananchi wetu.
2.
UMEME
Katika
ziara yetu suala la umeme nimeulizwa mara nyingi zaidi kwenye kata zote.
Wananchi waliuliza mikakati gani iliyopo ya kuwapatia umeme kwenye maeneo yao?
Wapo pia ambao walitaka kujua waliopisha mradi ya umeme watalipwa lini fidia
zao?
Umeme
kwenye jimbo la Bukombe umetekelezwa kwa mradi wa umeme wa Electricity V. Mradi
huu unatokana na mkopo wa fedha kutoka Benki ya maendeleo ya Africa (ADB)
ambao, ulilenga kuvipatia umeme vijiji saba (7) tu wilayani kwetu ambavyo ni Ituga,
Bukombe, Lyambamigongo, Ushirombo, Buntubili, Msasa na MJI wa Runzewe lakini
kutokana na mahitaji ya umeme tulipeleka maombi maalumu tukaongezewa vijiji
vingine 7 na kufanya jumla ya vijiji 14 vitakavyonufaika
na mradi wa elcticity V. Mradi huu umekamilika na sasa zoezi la usambazaji ndilo linaendelea kwenye miji ya ushirambo na Runzewe.
Kwakuwa
wilaya yetu haikuwahi kupata umeme wa REA awamu zote mbili zilizopita. Sasa
tumeomba nasi tuingizwe kwenye REA; nafurahi tumeingizwe kwenye mradi huu na
tayari vijiji vyetu vyote 53 kwenye kata 17 zitapata umeme na utafikia zaidi ya
vitongoji 176 kuanzia mwaka wa fedha ujao wa 2016/2017.
Kwakuwa
uunganishwaji wa umeme ni ghari. Wizara imetuletea teknolojia mpya ambao mteja
hatahitaji kuingia gharama ya kufanya wring kwanza ili kupokea umeme, chombo
kiitwacho UMETA, hiki kitapunguza gharma kwa wananchi wetu ili wabakiwe na
gharama ya kufungiwa mita mbayo ni shs 25,000/= tu na fomu ya maombi ni sh 6,000/=.
Imani
yangu nikuwa wananchi nao watajipanga
kumudu gharama ya mita ili baada ya
muda nyumba zetu Bukombe ziwe zimepata na zinatumia huduma hii muhimu ya
umeme.
Kuhusu
fidia tunalifuatilia jambo hili kwa karibu tunafahamu wapo wananchi 258 wanadai fidia mbalimbali za kupisha mradi wa umeme na
wanadai 149,000,000 na zoezi la ulipaji linaendelea vizuri bila shaka malipo
yataanza kulipwa kuanzia mwezi huu wa machi 2016.
Ninatoa
wito kwa wananchi kutokuibua madai mapya nje ya yale yaliyothaminiwa, maana
kufanya hivyo kunachelewesha upatikanaji na usambazaji wa umeme kwa watu wetu.
Wakati
tunamalizia ziara, wafanyakazi wa TANESCO walifanya mkutano na wanachi wa uyovu
kwenye mji wa Runzewe na kutoa taarifa kuwa watasambaza nguzo 25 tu. Jambo hili
likizua manung’uniko mengi Niliamua kumwalika Naibu Waziri wa Nishati na Madini
ambaye aliungana nasi kusikitika na hatimaye nguzo zimeongezwa kutoka 25 hadi
176. Hatua hii walau itafikia eneo kubwa zaidi la wananchi wa Uyovu na patakapo
baki patamaliziwa na mradi wa REA.
Kwasasa
nguzo zinaendelea kusambazwa Ushirombo na Uyovu ili kuwapatia umeme wananchi
wengi zaidi.
3.
WACHIMBAJI
WADOGO
Uchumi
wa wilaya yetu umejengwa na uchimbaji wa dhahabu. Haishangazi kuona wanachi
wengi zaidi wakiuliza juu ya wachimbaji wadogo.
Tumechukua
hatua za kuleta suluhu ya kudumu kwa
wachimbaji wetu. Mazumgumzo tumefanya na mgodi wa STAMIGOLD wa Tulawaka Biharamulo
ili waachie sehemu ya leseni zao ambazo hawazifanyii kazi tuwapatie wananchi (wachimbaji wadogo
wadogo) waweze kuendesha shughuli zao.
Sisi
wabunge wa Bukombe na Biharamlo tulifanya kikao
na uongozi wa mgodi kwa siku mbili tarehe 17/02/2016 na 18/02/2016 mbapo
tulikubaliana kulipa msukumo jambo hili. Tayari tumeshawasiliana na wizara juu
ya makubaliano yetu wizara imeyapitia mapendekezo yetu bila shaka utaratibu wa
namna gani utatolewa zoezi hili
litekelezwe zaidi kwaajili ya watu wetu.
Wito
wangu kwa wachimbani wadogo sasa wafikirie kujiunga kwenye vikundi ili
umilikishaji ukianza tuwe na mazingira mazuri ya kuanza kazi badala ya
maandalizi.
Naibu
waziri pia alipotutembelea pale Uyovu alituhakikishia anaenda kulifanya kazi
kwa haraka ili kazi ianze mapema.
Ninatoa
wito kwa wananchi kuwa na subira wakati tukilifuatilia jambo hili.
4.
ELIMU
Masuala
ya elimu pia yaliulizwa na kwakweli yalitupa mwanga kuwa mwamko wa elimu
wilayani kwetu unakuwa kwa kasi zaidi. Tumebaini mengi sana ya uelewa naya
kufanyia kazi.
Masuala
ya uhaba wa walimu wa shule za msingi ambapo wilaya yetu inaupungufu wa walimu
436, hata hivyo idadi inaweza kuongezeka zaidi kutokana na idadi kubwa zaidi ya
wanafunzi wa darasa la kwanza kuandikishwa kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko
matarajio yetu kutokanana mwitikio wa elimu bure.
Kwenye
shule za sekondari pia kwa uhaba wawalimu wa sayansi; shule nyingine hazina
hata mwalimu mmoja wa sayansi; tunapambana kuleta walimu wengine kwenye ajira ya walimu ijayo.
Elimu
bure imezaa changamoto za upungufu wa madarasa na madawati. Shule ya Ibamba
ndiyo inayoongoza kwa mkoa wa Geita kwa kuandishaji watoto wengi zaidi ambapo
zaidi ya watoto 1800 wameandikishwa.
Uwepo
wa changamoto hizi lazima tufikiri zaidi namna ya kuzitatua, tunaamini
tutaendela kuboresha kadri tunavyoendea.
Walimu
wetu wanamadai yao, ambayo kwa muda
mrefu hayajafanyiwa kazi, mathalani:-
a. Madai
ya kutokupandishwa madaraja kwa wakati
b. Kutorekebishiwa
mishahara yao kwa wakati na malimbikizo ya mishahara yao kutokulipwa kwa wakati
c. Walimu
wapya kutokupatiwa namba zao za ajira TSD numbers pamoja na vitambulisho vya
kazi hawajapatiwa
d. Kada
hii haijapata motisha yoyote toka kwa mwajiri
e. Wapo
walimu waliopelekwa kwenye mifuko ya
hifadhi ya jamii ambayo si machaguo yao.
Baada
ya ziara hii yapo ambayo kwa haraka tuliamua kuyachukulia hatua.
Upandishwaji
wa madaraja, tuliwasiliana na ofisi husika na wataanza kupandishwa waliogota muda
mrefu wapo walimu 145 tu watakao pandishwa kwa sasa.
Namba
za TSD tumewaomba wazifuate mkoani haraka na tayari zitaanza kusambazwa wiki ya
pili ya mwezi machi.
Ama
kuhusu motisha, tunafanya mazungumzo na makampuni ambayo yanaweza kuwakopesha
walimu vyombo vya usafiri. Imani yangu
hilo likifanikiwa litatupa hatua zaidi kwa walimu na watumishi wengine.
Tumeitaka
ofisi ya utumishi ipeleke haraka watumishi kwenye mifuko waliyochagua, bila
shaka hilo litatekelezwa mapema.
5.
MALI
ASILI
Wananchi
wengi wanokaa kando kando ya hifadhi wametoa malalamiko mengi juu ya mahusiano
mabaya kati yao (wananchi) na wahifadhi wa misitu na maliasili nyingine kwenye pori la kigosi.
Kuna taarifa za watu wanaotozwa mamilioni ya fedha kama rushwa, wanapigwa, wapo
wamepata ulemavu na wengine wamenyang’anywa mali zao.
Tumeyapokea
na kwakweli tunalaani sana unyanyasaji unaofanywa kwa wananchi, wahifadhi wanapaswa kufuata sheria
ingawa watekelezaji wa sheria wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria
pia.
Vitendo
vya kuomba rushwa, kupiga wananchi na unyang’anyi wa mali za wananchi si utekelezaji
wa sheria bali ni wizi na “uhuni’ kama
uhuni mwingine
Tumeomba
waziri wa maliasili utalii atembelee jimbo letu ili nae asikie mwenyewe manyanyaso haya kwa wananchi.
6.
MILIONI
HAMSINI ZA WANAWAKE, VIJANA ZA KILA KIJIJI.
Suala
hili limeulizwa sana, walau swali moja kwa kila makutano liliulizwa juu ya
upatikanaji wa fedha hizo
Ahadi
hii itatekelezwa na kuanzia mwaka ujao wa fedha 2016/2017 serikali italeta
utaratibu wa namna gani fedha hizo zitapatikana
tumewaomba wananchi na hasa akina mama wawe na subira wakati jambo hili
linafanyiwa kazi.
7.
TOZO
ZA MAFUNDI SELEMALA.
Mafundi
selemala kwenye wilaya yetu; wana malalamiko mengi juu ya tozo kubwa
zinazodaiwa na Halmashauiri mfano. Kitanda kimoja kinatozwa hadi shs 120,000
kiasi hiki ni kikubwa mno, ukilinganisha
na uwezo wa wateja wao.
Bahati
njema hata mkuu wa mkoa nae alishalifanyia kazi kwa kulitolea maelekezo ya
kupunguza gharama hizo.
8.
KILIMO
NA UFUGAJI
Wakulima
wetu hasa wa pamba, hawajafurahishwa na kilimo cha mkataba. Kilimo cha mkataba
kimesababisha bei ya mazao yao haipandi
na kwamba pembejeo haziletwi kwa wakati.
Kikao
cha RCC kilichoketi kilielekeza ununuzi wa pamba utakapoanza kila mnunuzi apate
nafasi sawa ya kununua, mfumo wa msimu uliopita hatatumika tena isipokua kwa
wakulima walioingia wenyewe kwenye mikataba.
Wafugaji
kama ilivyo sehemu nyingine hapa nchini wafugaji hawana maeneo ya kulishia
mifugo suala hili tutaendelea kulifanyia kazi, kitaifa na kiwilaya ili tutoe
ahueni kwa wafugaji wetu.
9.
Huduma
za Afya
Wananchi
wengi kwenye mikutano yetu wameomba uwepo wa huduma za Afya karibu zaidi na
wao, aidha wanasikitishwa sana ukosefu wa madawa kwenye vituo vya kutolea
huduma.
Nimewaomba
watuvumilie tunalifanyia kazi maana pamoja na kua limeibuka jimboni ni tatizo
hili limekua kila mahali hapa nchini. Tunaenda kwenye bajeti tutalisema kwa
nguvu zote.
Siku
20 jimboni zimenipa somo, zimenipa picha
ya kila kinachoendelea jimboni. Nimewaona mama zangu, baba zangu na ndugu zangu
na dada zangu ambao wana kiu ya haki ya maendeleo. Wananachi wanatamani kero
hizi ziondoshwe, wanatamani maisha bora kupitia raslimali ambazo Mungu aliwapa,
wanatamani wapate majawabu ya kero hizo!
Wananchi
wamenipa somo kuwa kama mbunge wajibu wa mbunge ni kuwa sauti ya wananchi na
daraja kati yao na serikali, nami kama mbunge nitahakikisha muunganiko huo
unakuwepo wakati wote.
Binafsi
kama mbuge, nitaendelea kuwa na wanabukombe wakati wote. Nawasihi waendelee
kunipa ushirikiano nitawaambia ukweli tupu. Na waniombee nami nitawaombea, ili
pamoja tujenge Bukombe yetu.
Kusema na kutenda, uwe Msingi Wetu Sote.
Comments
Post a Comment