Hayati Edward Sokoine, Waziri Mkuu aliyekufa huku akiacha mashati matatu na viatu ‘pea’ 2 tu


Na Charles Charles

SAA 10.00 jioni ile ya Aprili 12, 1984, Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), sasa Redio ya Taifa ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ilikatiza ghafla matangazo yake ya kawaida, kisha ukapigwa wimbo wa taifa wa “Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania…” 

Baada ya wimbo huo kumalizika huku wasikilizaji waliokuwa karibu na redio iwe nyumbani, ofisini na sehemu nyingine wakishangaa na kutaka kujua kwamba kuna nini, wote walipigwa bumbuwazi zaidi waliposikia sauti nzito, sauti ya huzuni na isiyokuwa katika ubora na madoido yake walivyoizoea ikieleza:
 

“Ndugu wananchi, leo saa saba mchana, ndugu yetu na kijana wetu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Edward Moringe Sokoine alipokuwa akisafiri kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam, gari yake ilipata ajali. Amefariki dunia!”
 

Ilikuwa hotuba fupi kuliko zote zilizowahi kutolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tangu akiwa Rais wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), Waziri Mkuu wa Serikali ya Madaraka ya Ndani (ya Tanganyika), Waziri Mkuu wa Tanganyika huru, Rais wa Tanganyika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hata vinginevyo.
 

Ilikuwa ni fupi kuliko zote ikiwa ni ya kwanza na ya mwisho kwake kwa taifa na hata kimataifa, hotuba ambayo hadi leo imebaki ni rekodi katika maisha yake yote akiwa ni kiongozi wa kitaifa na kimataifa.
 

Hotuba hiyo ilileta jitimai na simanzi kubwa nchini ambapo kwa mfano, akina mama waliokuwa wakiuza maandazi na vitumbua katika eneo la Mtoni Kwa Azizi, Temeke jijini Dar es Salaam ‘walichanganyikiwa’, wengi wakajikuta wakisahau biashara zao na kuanza kukimbia ovyo mitaani huku wakiangua vilio vya kufiwa na mpendwa wao.
 

Kana kwamba haitoshi, kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Taifa ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kilichokuwa kikifanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, kilisambaratika bila kuahirishwa baada ya Mwenyekiti wake ambaye sasa ni hayati, Sofia Kawawa kuwatangazia wajumbe kuhusu msiba huo mzito na wa ghafla mno.
 

Kina mama hao wote, kila mmoja utadhani wameamrishwa waliangua kilio kama mtoto aliyekutana na paka mwenye vichwa saba usiku wa manane, kisha wakaondoka na kuachana kama wanyama bila ya kuagana.
 

Aidha, mwanaume mmoja aliyekuwa akisubiri usafiri wa daladala katika Kituo cha Posta ya Zamani, katikati ya jiji hilo la Dar es Salaam naye alisikika akisema: “Ni bora hata angekufa baba yangu mzazi kuliko kufa kwa Sokoine!”
 

Edward Moringe Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tatu wa nchi hii alizaliwa Agosti Mosi, 1938 huko Monduli Juu, wilaya ya Monduli mkoani Arusha katika familia ya kifugaji.
 

Aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara yake ya kwanza Februari 13, 1977 na kutumikia nafasi hiyo hadi Novemba 7, 1980 alipojiuzulu na kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Sofia, Bulgaria.
 

Aliporejea nchini miaka miwili baadaye aliteuliwa tena kushika wadhifa huo Februari 24, 1983 na kuendelea nao hadi alipokufa kwa ajali Aprili 12, 1984 katika eneo la Dakawa (ambalo sasa lipo wilaya ya Mvomero) mkoani Morogoro.
 

Kifo chake hicho ambacho kilitokea alipokuwa akisafiri kutoka katika kikao cha bunge mjini Dodoma, kilisababishwa na benzi alilokuwa akisafiria kugongwa uso kwa uso na gari aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa ikiendeshwa na mpigania uhuru wa chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini, Dumisan Dube.
 

Wakati alipokufa, Sokoine tayari alikuwa amejitengenezea taswira ya uzalendo mkubwa kabisa kwa nchi yake, yule ambaye hadi leo inaaminika kuwa ukimwondoa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hakuna kiongozi mwingine yeyote wa kisiasa au wa umma aliyefikia uchapakazi wake, uadilifu wake, utendaji wake na hata vinginevyo.
 

Katika hotuba yake ya mwisho kwa taifa alipokuwa akiahirisha kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma hapo Aprili 11, 1984 alisema:
 

“Ni kheri mkulima atakayekamatwa akiiba mbolea ili (aende) akaitumie vizuri shambani kwake, huyo (tukidhibitisha hivyo) tutamsamehe, lakini ole wake kiongozi atakayekamatwa kwa (tuhuma za) kufanya ubaridhifu wa mali ya umma”.
 

Kauli hiyo thabiti katika hali zote ilikuwa ikitoka kinywani mwa mtu na kiongozi aliyekuwa akichukia sana rushwa, ubinafsi na wizi wa fedha za serikali.
 

Ilitoka mdomoni mwa Waziri Mkuu aliyekuwa akisimamia kauli zake, yule ambaye kile anachosema ndicho alichokuwa nacho moyoni na siyo kwa kuigiza kama wanavyofanya viongozi wengi serikalini, vyama vya siasa na sehemu nyingine za utawala na uongozi wa umma.
 

Aliishi maisha ya kawaida tofauti na wadhifa wake huo wa juu kabisa ukiwa ni wa tatu baada ya Rais, wakati huo akiwa ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Makamu wa Rais, kipindi ambacho alikuwa Ali Hassan Mwinyi ambaye sasa ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili.
 

Alikuwa hajikwezi wala kuishi tofauti na maisha wanayoishi wananchi walio wengi, hivyo ukiondoa tu itifaki za kiserikali alizokuwa ni lazima apewe hakuwahi kabisa kuishi kifahari kama wanavyoishi viongozi wa leo.
 

Ukiachilia mbali ‘utajiri’ wa ng’ombe alioachiwa urithi na wazazi wake kule Monduli, Sokoine kamwe hakuwahi kumiliki mali nyingine yoyote yakiwemo mavazi ya gharama.
 

Maisha yake hayo yaliwekwa hadharani na Rais Julius Nyerere wakati wa mazishi ya Waziri Mkuu huyo wa zamani huko Monduli aliposema:
 

“Edward Sokoine hakuwa na mali yoyote. Ukiacha ng’ombe alioachiwa urithi na wazazi wake alikuwa na mashati matatu, suruali tatu na viatu pea mbili!”
 

Nani kama yeye?
 

Bila hata kuwazungumzia mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya ama wabunge kamwe hakuna hata diwani, afisa mtendaji wa kata, mtaa au wa kijiji, mwalimu wa shule ya msingi wala karani tu wa masjala mwenye mashati matatu, suruali tatu na viatu pea mbili tu kama ilivyokuwa kwa Sokoine!
 

Leo viongozi wetu au watumishi wa serikali wanashindana kwa mavazi, tena ya gharama wakionyeshana nani anayevaa kuliko mwingine.
 

Wanatambiana kuwa nani anayevaa nadhifu kwa mashati, suruali, suti, viatu, saa au magauni, sketi, blausi na kusuka nywele za gharama kubwa zaidi kushinda wenzake na hata vinginevyo.
 

Yule anayebadilisha mashati yake matatu, suruali zake tatu, viatu pea mbili, magauni matatu, sketi tatu au blausi tatu huku akisuka nywele za kawaida au kunyoa siku zote anaonekana mshamba na mtu aliyepitwa na wakati!
 

Maisha yake hayo ya haki ndiyo yaliyompa jeuri ya kukemea aina zote za hujuma, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma kama alivyosema katika hotuba yake ile ya mwisho kwa taifa, Dodoma Aprili 11, 1984:
 

“Ole wao viongozi wanaotumia nafasi za madaraka yao ya umma (kwa ajili ya) kuiba, kuhujumu uchumi au kupokea rushwa maana salama yao ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu na labda nisiwajue”.
 

Mbali na maneno hayo mazito, Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye kifo chake kiliacha kila aina ya simanzi, majonzi na kumbubujisha machozi hadi Mwalimu Julius Nyerere alipouona mwili wake, Ikulu baada ya kufikishwa hapo kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam pia alisema, jana yake kule bungeni:
 

“Nasikia kuna viongozi wa umma huko mikoani wanagombania magari badala ya kugombania maendeleo ya wananchi, naagiza tabia hii ikome mara moja”.
 

Hayati Edward Sokoine anakumbukwa pia kwa kusimamia vita dhidi ya wahujumu uchumi kuanzia mwaka 1983 – 1984 alipokufa kwa ajali, ile ambayo hata hivyo “aliondoka nayo kaburini”.
 

Katika hotuba yake kwa Watanzania wakati wa mazishi ya kiongozi huyo yaliyofanyika nyumbani kwake kule Monduli Juu, Arusha, Baba wa Taifa, wakati huo akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa siri nyingine ambayo ni vigumu kukubalika.
 

Alisema kwamba kabla ya kifo chake hicho, Sokoine alilalamikia ukubwa wa baraza la mawaziri, hivyo akashauri lipunguzwe na kuwa dogo kulingana na mahitaji na uwezo wa taifa kiuchumi.
 

Ingawa ushauri huo ungeweza pia kutolewa na mtu mwingine yeyote, kilichomshangaza hata Mwalimu Nyerere ni kauli ya Sokoine kwamba likivunjwa na kuundwa upya, yeye mwenyewe alikuwa radhi na tayari kutoteuliwa tena kama rais huyo wa kwanza wa nchi hii angeona hamhitaji tena!
 

Sokoine aliyekufa kwa ajali akiwa na umri wa miaka 45, miezi minane na siku 12 kamili alianza elimu yake ya msingi mwaka 1948, kulekule Monduli, wakati huo ikiitwa wilaya ya Masailand alikosoma hadi darasa la nane.
 

Kutoka huko aliendelea na masomo katika Shule ya Sekondari Umbwe, Moshi mkoani Kilimanjaro alikohitimu darasa la 10 mwaka 1958 na kujiunga rasmi na chama cha TANU mwaka 1961.
 

Kuanzia mwaka 1962 – 1963 alisomea uongozi na utawala katika iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani Mashariki. Aliporejea nchini, wakati huo akiwa kijana mwenye umri wa miaka 25 aliajiriwa serikalini akiwa Afisa Mtendaji wa Wilaya ya Masailand.
 

Miaka miwili baadaye aligombea na kuchaguliwa kuwa mbunge wa wilaya hiyo ambayo sasa iliitwa Monduli, fursa iliyompa mwanya wa kuonyesha zaidi kipaji chake kikubwa katika uongozi na utumishi wa umma.
 

Ilikuwa kipindi hicho ndipo alipoteuliwa kuwa Waziri Mdogo wa Kazi, Mawasiliano na Uchukuzi mwaka 1967, kisha akateuliwa kuwa Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Rais (Usalama) ilipofika mwaka 1970.
 

Miaka miwili baadaye hapo mwaka 1972, Sokoine aliteuliwa na Rais Julius Nyerere kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa hadi Februari 13, 1977 alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kubadilishana nafasi na mtangulizi wake, Rashid Mfaume Kawawa.
 

Akiwa amechaguliwa kwa mara yake ya tatu mfululizo kuwa Mbunge wa Monduli mwaka 1975, Sokoine aliingia kwa mara ya kwanza pia katika ujumbe wa Kamati Kuu ya TANU, kisha akawa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM mpaka Novemba 7, 1980 alipojiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu kwa matakwa yake mwenyewe.
 

Alirejea katika chombo hicho cha juu kabisa kisiasa alipoteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa nchi hii ilipofika Februari 24, 1983 hadi Aprili 12, 1984 alipopata ajali ile barabarani, eneo la Dakawa, Morogoro na kufa papo hapo.
 

Katika kutambua mchango wake mkubwa kwa taifa, serikali ilikigeuza kilichokuwa Kitivo cha Kilimo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kampasi ya Morogoro na kuwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, maarufu kwa kifupi cha SUA.
 

Historia inaonyesha kwamba kilianzishwa mwaka 1964 kama Chuo cha Kilimo kilichokuwa kinafundisha na kutoa stashahada (au diploma) za kilimo, kisha kikapandishwa hadhi na kuwa Kitivo cha Kilimo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hapo mwaka 1969.
 
Akiwa ni kiongozi mwandamizi wa taifa, Sokoine anakumbukwa hadi leo, miaka 32 baada ya kifo chake siyo kwa sababu alikuwa Waziri Mkuu kwani wadhifa huo umeshashikwa pia na wanasiasa wengine akiwemo mrithi wake alipofuka mwaka 1984, Balozi Dk. Salim Ahmed Salim.
 

Wengine waliowahi kushika wadhifa huo ukimwondoa Mwalimu Julius Nyerere, Kawawa na Waziri Mkuu wa sasa, Majaliwa Kassim Majaliwa ni Cleopa David Msuya, Joseph Sinde Warioba, John Samwel Malecela, Frederick Tluway Sumaye, Edward Ngoyai Lowassa pamoja na Mizengo Kayanza Pinda.
 

Hayati Sokoine anakumbukwa hadi leo kwa sababu aliamini, kusimama na kupigana kwa vitendo ili kutetea haki kwa wote, usawa usiokuwa na ubaguzi pamoja na uwajibikaji kazini katika utumishi wa umma.
 

Alikuwa ni mzalendo wa kweli aliyeishi na kuamini katika misingi halisi ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, kiongozi ambaye wakati wake wote alikuwa mchapakazi na mtu asiyejua kujikweza.
 

Ndiyo maana alifanya kazi mpaka usiku wa manane na hata alipokuwa barabarani akipitia mafaili na nyaraka mbalimbali, akatoa maelekezo ya kufanya kwa wasaidizi wake kuanzia ofisini hadi mawaziri, wakuu wa mikoa na watendaji wengine serikalini.
 
Alikuwa akichukia na kupambana kwa nguvu zake zote dhidi ya vitendo vyote vinavyohusu ubadhirifu wa fedha na mali za umma, wizi wa aina zote, kutowajibika au uzembe kazini hususan katika utumishi wa umma, rushwa, uhujumu uchumi, ulanguzi pamoja na magendo.
 

Aliamini kuwa “Siasa ni Kilimo” na ndiyo maana siku zote aliipigania sekta hiyo kwa kauli na vitendo. Alitaka Tanzania ijitosheleze yenyewe kwa chakula, iiuze nje ya nchi ziada na kuzalisha kwa wingi mazao yote ya biashara kama ya pamba, kahawa, chai, mkonge, kakao na kadhalika ili kuliingizia taifa fedha za kigeni.
 

Alifanya hivyo akiamini pia kuwa kilimo ni uti wa mgongo. Hakutaka taifa liwe ombaomba ila lenye nguvu kiuchumi. Ndiyo maana alijitahidi kuliwekea msingi imara wa maendeleo kupitia elimu ya kujitegemea na siyo ya kutafutia kuajiriwa.
 

Ndiyo maana hadi leo, Jumanne Aprili 12, 2016 ikiwa ni miaka 32 kamili baada ya kifo chake kilichotokea kwa ajali ya barabarani Aprili 12, 1984, Watanzania bado wanazidi kumlilia utadhani amekufa jana na kushindikana kabisa kumsahau.
 
Mungu aendelee kuiweka roho yake mahali pema peponi. AMEN!


Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Itikadi na Uenezi katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0787 088 870

Comments

Post a Comment