UVCCM YAVITAKA VIKUNDI VINAVYODAIWA NA HALMASHAURI KUREJESHA MADENI KABLA YA KUKAMATWA

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Vikundi vinavyodaiwa kuwa na madeni ya mikopo iliyotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, vimetakiwa kurejesha mikopo hiyo kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe, Nelvini Ndugu, wakati wa ziara yake pamoja na Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), iliyolenga kukagua uhai wa Chama na Jumuiya zake katika Kata za Bulangwa na Katente.Katika ziara hiyo, viongozi hao pia walipokea na kujadili hoja mbalimbali zilizohusu vikundi kutopata mikopo ya Halmashauri, hali iliyochangiwa na baadhi ya vikundi kutorejesha mikopo waliyopewa.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika Kata ya Bulangwa, Ndugu aliwataka vijana kuacha uzembe na ujanja katika matumizi na urejeshaji wa fedha za mikopo ya Halmashauri, akisisitiza kuwa fedha hizo zinapaswa kurejeshwa ili ziweze kutumika kuwawezesha wananchi wengine.Alisema mikopo hiyo si fedha za kupewa bure, bali ni fedha za Serikali zinazotakiwa kurejeshwa na kukopeshwa kwa makundi mengine yenye uhitaji.

“Vijana tuache ujanja katika fedha za mikopo ya Halmashauri. Kama tumekopa, tunapaswa kurejesha kwa wakati. Tusisubiri mpaka Serikali ichukue hatua za kisheria ndipo turejeshe fedha,” alisema Ndugu.Akiwa Kata ya Katente, Ndugu alielezwa kuwa kata hiyo imeondolewa katika mpango wa kupokea mikopo kutokana na baadhi ya vikundi kuwa na madeni na kutorejesha fedha walizokopa.

Alisisitiza kuwa Serikali haiwezi kufumbia macho madeni ya mikopo, akisema hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa ili fedha hizo ziweze kurejeshwa na kutumika kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wengine.Awali, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Bukombe, Stamil Mcharo, aliwataka vijana kuendelea kuhamasishana na kushirikiana katika kutekeleza majukumu ya Jumuiya hiyo.Mcharo alisema UVCCM inafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Serikali, hivyo kila wanapofanya ziara katika kata wanatarajia wataalamu wa kata kuwepo ili kujibu hoja na kusaidia kutatua kero zinazowakabili wananchi, hususan zinazohusu mikopo.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Bulangwa, Nkuba Ndonje, alisema kata hiyo ina jumla ya vikundi 24 miongoni mwa vikundi hivi vimemaliza marejesho ya mikopo na vimeanza kuchukua mikopo mingine.Alisema pia kuna vikundi vinne vilivyofikia hatua za mwisho za kumaliza marejesho, huku kukiwa na vikundi vingine vinavyoendelea kufuatiliwa ambavyo kwa pamoja vinadaiwa kiasi cha Sh 54.1milioni.

Ndonje alisema pia amefuatilia baadhi ya vikundi vilivyokopa fedha tangu mwaka 2013 na nyuma yake, ambapo baadhi yao tayari wameanza kurejesha madeni yao.Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Bulangwa, Alex Maricel, aliwashukuru viongozi wa UVCCM kwa kuwafikia vijana na kuwasikiliza, akiwataka kuendelea kuwalea na kuwafundisha vijana misingi na maadili mema ya Chama.Maricel alisema atahakikisha anatekeleza maelekezo yaliyotolewa na viongozi hao, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha vijana kurejesha mikopo ya Halmashauri.Pia aliwaomba viongozi wa Chama katika kata hiyo kuendelea kuwakumbusha vijana majumbani umuhimu wa kushirikiana katika shughuli za Chama kwa lengo la kufikia malengo yaliyowekwa.

Akizungumzia hali ya mikopo katika Kata ya Katente, Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Elias Belege, alisema kata hiyo ina vikundi sita vinavyodaiwa zaidi ya Sh milioni 37.Belege alisema amepokea hati za wito wa baadhi ya wadaiwa kufikishwa mahakamani, ikiwa ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa.Alisema amekuwa akifuatilia baadhi ya wadaiwa, huku wengine wakiwa wamekuwa wakitafutwa bila mafanikio, hali ambayo imechangia vikundi vingine vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kukosa fursa ya kupata mikopo.Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM Kata ya Katente, Kanu Hezron, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo katika kata, Devid Jeremia, alisema wamefarijika kufikiwa na viongozi wa UVCCM na kupewa maelekezo mbalimbali.Hezron alisema vijana wa Kata ya Katente wataendelea kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao katika shughuli za Chama na maendeleo ya jamii.

Comments