UVCCM WAMPONGEZA AFISA MAENDELEO YA JAMII


Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, umempongeza Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Runzewe Mashariki, Vumilia Mchwampaka, kwa juhudi zake za kuhamasisha uundaji na uendelezaji wa vikundi vinavyonufaika na mikopo isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe, Nelvin Ndugu, wakati wa ziara yake katika Kata ya Runzewe Mashariki, akiwa ameambatana na kamati ya utekelezaji  kwa lengo la kuona uhai wa chama na jumuiya zake pamoja na kupata taarifa kuhusu namna vijana wanavyonufaika na mikopo inayotolewa na halmashauri.Ndugu alisema amefanya ziara katika kata mbalimbali na kubaini kuwa baadhi ya maeneo bado yanakabiliwa na changamoto katika kuendesha vikundi, lakini ameipongeza Kata ya Runzewe Mashariki kwa kuwa na vikundi vinavyofanya vizuri.

“Nimepita katika kata mbalimbali na nimeona baadhi ya maeneo yanachechemea, lakini Runzewe Mashariki nimefurahi. Nimpongeze sana Afisa Maendeleo ya Jamii kwa kuwaunganisha vijana, kuwasajili katika vikundi na kuwawezesha kupata mikopo. Jambo kubwa zaidi ni kwamba vikundi hivi vimefanya marejesho vizuri,” alisema Ndugu.Alisema juhudi hizo zinapaswa kuendelezwa kwa kuhakikisha vijana wanaendelea kupewa elimu na kuhamasishwa kutumia fursa zinazotolewa na serikali ili kujikwamua kiuchumi.

Aidha, aliwaomba viongozi wa serikali na chama kuendelea kuwaunga mkono viongozi mbalimbali, akiwemo Mbunge wa Bukombe, Dkt. Doto Biteko, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za kuleta maendeleo kwa wananchi.Awali, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Runzewe Mashariki, Vumilia Mchwampaka, alisema alipoanza kazi katika kata hiyo mwaka 2024 alikuta vikundi vitano, ambavyo kwa juhudi za uhamasishaji vimeendelea kuongezeka hadi kufikia vikundi nane.

Mchwampaka alisema vikundi hivyo vimenufaika na mikopo isiyo na riba kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe yenye thamani ya shilingi milioni 89, huku vikundi hivyo vikifanya marejesho vizuri.

Aliwataka vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Bukombe kwa kuunda vikundi na kuanzisha shughuli za uzalishaji zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Runzewe Mashariki, Mery Nchiba, alisema pamoja na vikundi kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, kata hiyo imepokea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya shilingi milioni 157.Alisema kati ya fedha hizo, shilingi milioni 60 zimetokana na mapato ya ndani ya halmashauri.Nchiba aliwataka wananchi, wanachama wa CCM na watumishi wa umma kuendelea kushirikiana katika kusimamia maendeleo ya kata hiyo na kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.Alisema maendeleo yanayoendelea kuonekana katika maeneo mbalimbali yanatokana na ushirikiano wa viongozi na serikali, akimtaja Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kusukuma mbele ajenda za maendeleo, pamoja na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya huduma kwa wananchi.

Ziara hiyo ya Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe ilihusisha pia Kata za Busonzo, Runzewe Mashariki na Ng'anzo, ambapo alikutana na viongozi na vijana na kupata taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli za jumuiya hiyo.Akiwa Kata ya Ng'anzo, Katibu wa UVCCM Tawi la Kazibizyo Luyangana, Hames, alimpongeza Mwenyekiti huyo kwa ziara yake, akisema ziara yake ya mwaka 2014 ilihamasisha vijana kuunda vikundi.Alisema baada ya hamasa hiyo, vijana waliunda kikundi na kupata mkopo wa shilingi milioni 14, ambao tayari wamefanikiwa kuurejesha na sasa wanamiliki pikipiki zinazowasaidia katika shughuli zao za kiuchumi.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe, Nelvin Ndugu, aliwataka vijana hao kutumia uzoefu walioupata katika mkopo wa kwanza kuomba mkopo mwingine ili kukuza zaidi shughuli zao za kiuchumi.Alisema vijana wanapaswa kujenga biashara na shughuli zenye uwezo wa kukua na baadaye kuwa vyanzo vya ajira kwa vijana wengine katika jamii.

Comments