Timu ya Ushirombo Warriors FC imefanikiwa kutinga fainali ya KNK CUP 2026 ya Wilaya ya Bukombe baada ya kuifunga Msasa FC kwa mikwaju ya penalti 5-3, katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Ushirombo.
Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa, huku timu zote mbili zikianza kwa tahadhari na umakini, kila upande ukifanya mashambulizi ya kushtukiza katika kutafuta bao la kuongoza.
Hata hivyo, licha ya juhudi za wachezaji wa pande zote mbili, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika bila bao, huku timu hizo zikienda mapumziko zikiwa sare ya 0-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi, ambapo Ushirombo Warriors FC na Msasa FC ziliongeza mashambulizi na kuufanya mchezo kuwa wa kuvutia, huku kila timu ikitafuta nafasi ya kuvunja ukuta wa mpinzani wake.
Dakika 90 zilipokamilika bila timu yoyote kupata bao, mwamuzi wa kati Seleman Juma aliamuru kupigwa kwa mikwaju ya penalti ili kumpata mshindi wa mchezo huo wa nusu fainali.
Katika mikwaju hiyo ya penalti, Ushirombo Warriors FC walionyesha umakini mkubwa na kutumia vyema nafasi walizopata, na hatimaye kuibuka na ushindi wa 5-3 dhidi ya Msasa FC, hivyo kujihakikishia tiketi ya kucheza fainali ya KNK CUP 2026.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya KNK CUP 2026, Joseph Kabote, alisema Ushirombo Warriors FC watakutana na Katome FC katika mchezo wa fainali utakaochezwa Jumatatu, Septemba 7, 2026.
Kabote alisema jina KNK ni kifupi cha “Kusema Na Kutenda”, ambalo ni kaulimbiu ya mdhamini wa mashindano hayo, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.
Alisema Dkt. Biteko amekuwa akidhamini mashindano hayo tangu mwaka 2016 hadi sasa, hatua inayolenga kuendeleza vipaji vya vijana kupitia michezo katika Wilaya ya Bukombe.
Katika siku hiyo ya fainali, Msasa FC pia itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Bukombe Stadium kuikabili Bugelenga FC katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu ya KNK CUP 2026.
Fainali ya KNK CUP 2026 inatarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa, huku Ushirombo Warriors FC na Katome FC zikiwa zimefika hatua hiyo baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika safari yao ya mashindano.

Comments
Post a Comment