USHIROMBO WARRIORS FC WATWAA UBINGWA WA WILAYA KNK CUP 2026


Na Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Timu ya Ushirombo Warriors FC imetwaa ubingwa wa Wilaya katika mashindano ya KNK CUP 2026, baada ya kuichapa Katome FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Bukombe Stadium.Mchezo huo wa fainali umechezwa katika Uwanja wa Bukombe Stadium uliopo Mtaa wa Kilimahewa, Kata ya Katente, Tarafa ya Ushirombo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, huku Ushirombo Warriors wakionyesha kiwango kizuri na kutumia vyema nafasi walizopata.Ushirombo Warriors FC walipata bao la kwanza dakika ya 43, kupitia kwa mshambuliaji wao Hames Kigwangala, aliyefanikiwa kuipatia timu yake uongozi kabla ya mapumziko.Kipindi cha pili, Katome FC walirejea uwanjani kwa kasi wakisaka bao la kusawazisha, huku wakifanya mashambulizi kadhaa kuelekea lango la Ushirombo Warriors.Hata hivyo, safu ya ulinzi ya Ushirombo Warriors iliendelea kuwa imara na kuzuia mashambulizi ya Katome FC.Dakika ya 59, Hames Kigwangala alifunga bao lake la pili na kuifanya Ushirombo Warriors kuongoza kwa mabao 2-0.Katome FC waliendelea kusaka mabao ya kurejea mchezoni, lakini hawakuweza kupata bao hadi dakika 90 za mchezo zilipokamilika.Baada ya ushindi huo, Ushirombo Warriors FC walitangazwa kuwa mabingwa wa Wilaya wa mashindano ya KNK CUP 2026, yanayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.Kama mabingwa, Ushirombo Warriors FC walikabidhiwa Kombe, seti tatu za jezi, mipira mitatu pamoja na kitita cha shilingi milioni 5.Katome FC, ambao walimaliza nafasi ya pili, walikabidhiwa seti mbili za jezi, mipira miwili pamoja na shilingi milioni 3.Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Msasa FC, ambao walikabidhiwa seti moja ya jezi, mpira mmoja pamoja na shilingi milioni 1.Zawadi hizo zilikabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskasi Muragili, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.Akizungumza katika hafla hiyo, Mratibu wa Kamati ya Mashindano ya KNK CUP 2026, Wilaya ya Bukombe Bosco Mwidad, alisema mashindano hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaibua vijana wenye vipaji vya soka.

Mwidad alisema tangu mashindano hayo yalipoanza mwezi Julai mwaka huu, jumla ya timu 248 zilishiriki, huku zawadi zikitolewa kuanzia ngazi ya kata hadi tarafa. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadis Paskasi Muragili, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, alimpongeza mdhamini wa mashindano hayo, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kuyaunga mkono.

Alisema KNK CUP imekuwa chachu ya kuibua vipaji na kutoa fursa kwa vijana kuweza kusajiliwa katika timu zinazoshiriki madaraja ya juu nchini.“Niko hapa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa. 

Amempongeza Mbunge kwa kuendelea kudhamini mashindano haya na anatamani kupitia KNK CUP ipatikane timu itakayocheza Ligi Kuu Tanzania Bara, ili Mkoa wa Geita tuwakilishwe na timu zaidi ya moja,” alisema Muragili.

Mhadis Muragili pia alisema mashindano hayo yamekuwa na mchango katika kukuza uchumi wa wananchi, kwani yanapowakutanisha watu kutoka maeneo mbalimbali, wafanyabiashara hupata fursa ya kufanya biashara wakati wa michezo.Nahodha wa Ushirombo Warriors FC, Damas Buyenze, alieleza furaha yake baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Wilaya kwa mara ya kwanza.

Buyenze alimshukuru Mungu kwa kuwawezesha kufika hatua hiyo, huku akiwapongeza wachezaji wenzake kwa kujituma na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi.

“Nina furaha sana pamoja na wachezaji wenzangu kwa kutwaa ubingwa wa Wilaya, kwani si jambo dogo. Tulijipa moyo, tukajituma na kumsikiliza mwalimu wa timu, na leo tumetwaa ubingwa. Pia namshukuru Mungu kwa kunisaidia kuwa golikipa bora", alisema Buyenze. Nahodha wa Katome FC Paschal Paul alisema matokeo wameyaokea na wamefungwa kutokana na makosa hivyo watajipaga mwaka kesho watapambana kusaka Ubingwa tena. 

Comments