Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexzander Mnyeti, amesema kipaumbele chake katika uongozi wake ni kuhakikisha wananchi, hususan wenye kipato cha chini, wanapata huduma stahiki na kero zao zinatatuliwa kwa wakati.
Mnyeti amesema wananchi ndio msingi wa uwepo wa Serikali, hivyo amewataka watumishi wa umma katika Mkoa wa Geita kuhakikisha wanawahudumia wananchi kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma.
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa kauli hiyo Septemba 18, 2026, wakati akizungumza na watumishi wa umma wa kada mbalimbali pamoja na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, katika ziara yake ya kwanza ya kujitambulisha baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Aliwataka watendaji wa vijiji na kata kuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuzitatua kabla ya kero hizo kufikishwa kwa viongozi wa ngazi za juu.
“Kila mtumishi wa umma ashughulikie changamoto za eneo lake. Nimeenda Kata ya Uyovu, nimekuta wananchi 20 wamejitokeza na changamoto na kero ambazo hazijatatuliwa. Hali hii haitakiwi katika Wilaya ya Bukombe wala Mkoa mzima wa Geita,” alisema Mnyeti.
Alisema hatasita kuchukua hatua dhidi ya mtumishi ambaye atashindwa kuwahudumia wananchi na badala yake wananchi wakawa wanamlalamikia mara kwa mara.
“Katika uongozi wangu wa Mkoa wa Geita, kipaumbele changu ni kusikiliza matatizo ya wananchi na kutatua kero zao. Nikija kwako Afisa Mtendaji wa kijiji au kata ukalalamikiwa na wananchi na wao wakakulalamikia, haki ya Mungu nitaondoka na wewe,” alisema.
Mnyeti pia aliwataka watendaji wa vijiji na kata kuanza kuitisha mikutano ya hadhara kwa ajili ya kutoa taarifa za mapato na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Aidha, aliwataka watumishi wa umma kujenga uhusiano mzuri na wananchi, huku akisisitiza kuwa katika ziara zake zijazo atatembelea miradi ya maendeleo ili kujionea utekelezaji wake.
“Nendeni mkajipendekeze kwa wananchi. Leo sizungumzii miradi, nitarudi na nitapita kuiona,” alisema.Katika hatua nyingine, Mnyeti aliwataka watumishi wa umma kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wawe wabunifu, huku wakizingatia sheria, taratibu na kanuni ili kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
Mnyeti pia aliwapongeza wananchi wa Bukombe kwa kumuamini na kumchagua Mbunge wa Jimbo hilo, Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, akisema amekuwa akifanya jitihada za kuleta miradi ya maendeleo na kuchangia mabadiliko katika wilaya hiyo.
Akitoa salamu za Dkt. Biteko kwa wananchi wa Bukombe, Mnyeti alisema mbunge huyo alitamani kuwepo katika ziara hiyo, lakini alikuwa nje ya nchi kutokana na majukumu aliyokuwa akiyatekeleza.
“Dkt. Biteko anawasalimia sana wananchi wa Bukombe. Alitamani kuwepo hapa leo, lakini kwa sababu ya majukumu aliyonayo yuko nje ya nchi. Anawapenda na anawasalimia sana,” alisema Mnyeti.
Mnyeti pia aliwataka viongozi na watendaji kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo inasimamiwa na kujengwa kwa ubora unaostahili.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, alimpongeza Dkt. Doto Biteko kwa juhudi anazofanya katika kuleta maendeleo wilayani Bukombe.
Kingalame alisema tangu Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iingie madarakani, Wilaya ya Bukombe imeendelea kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Kingalame, katika sekta ya elimu, idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 80 hadi 103, sawa na ongezeko la shule 23, huku shule za sekondari zikiongezeka kutoka 16 hadi 30.
Akizungumzia sekta ya afya, alisema idadi ya zahanati imeongezeka kutoka nane hadi 23, huku vituo vya afya vikiongezeka kutoka vitatu hadi saba.
Alimpongeza Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Bukombe.Kuhusu huduma ya maji, Kingalame alisema wakati Serikali ya Awamu ya Sita ikiingia madarakani, upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya mjini ulikuwa asilimia 47, lakini umefikia asilimia 68.
Alisema katika maeneo ya vijijini, upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 28 na sasa umefikia asilimia 66.Katika sekta ya nishati, alisema idadi ya vijiji vilivyokuwa vimefikiwa na umeme imeongezeka kutoka vijiji 59 hadi 64, huku akieleza kuwa vijiji vyote 64 kwa sasa vina umeme.
Kingalame alisema mtandao wa barabara wa Walami ulikuwa na urefu wa kilomita tatu, lakini sasa umefikia kilomita 9.9.Aidha, alisema mtandao wa barabara wa Chagalawe umeongezeka kutoka kilomita 193.3 hadi kilomita 478.6.
Kuhusu fedha za maendeleo, Kingalame alisema Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe katika mwaka wa fedha 2025/2026 ilipokea takribani Sh bilioni 16.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo miradi katika sekta ya elimu, miundombinu na miradi ya kimkakati.
Alisema fedha hizo zimetumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa shule za msingi na sekondari, mitihani, miundombinu, miradi ya kimkakati, pamoja na miradi mingine inayotekelezwa na Halmashauri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutembelea wilaya hiyo na kukutana na watumishi pamoja na wananchi.Mfikwa alisema maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa yamepokelewa na watumishi na watahakikisha yanatekelezwa.
Alisema watumishi wako tayari kushirikiana na Mnyeti katika kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kufika katika vijiji mbalimbali na kuhakikisha kero na changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi.

Comments
Post a Comment