Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, amepiga marufuku walimu wa shule za msingi na sekondari kupokea fedha kutoka kwa wanafunzi zinazodaiwa kuwa michango ya wazazi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo shuleni, ikiwemo ununuzi na ufungaji wa vifaa vya kinga dhidi ya radi.
Mnyeti ametoa maelekezo hayo Septemba 18, 2026, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ofisi ya CCM Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kwanza ya kujitambulisha kwa wananchi, kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili.
Hatua hiyo imekuja baada ya Afisa Elimu kuulizwa kuhusu malalamiko ya wananchi, hususan wazazi wa wanafunzi katika Kata ya Igulwa, ambao wamekuwa wakidaiwa kuchangia Sh4,000 kwa kila mwanafunzi kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kinga dhidi ya radi shuleni.
Hoja hiyo iliwasilishwa Ramadhan Hussen na mwanafunzi wa Shule ya Amani, Daniel Charle, aliyeomba msaada kwa Mkuu wa Mkoa akieleza kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikabiliwa na adhabu shuleni ikiwemo kuchapwa viboko pale wanaposhindwa kupeleka fedha hizo kutoka kwa wazazi wao.
Baada ya kusikiliza hoja hiyo, Mnyeti alisema wanafunzi hawapaswi kutumwa na walimu kwenda kuomba au kupeleka fedha za michango kutoka kwa wazazi wao.
Alisema endapo wazazi watakubaliana kupitia vikao vyao kuchangia fedha kwa ajili ya maendeleo ya shule, wazazi wenyewe wanapaswa kuunda kamati itakayohusika na ukusanyaji pamoja na usimamizi wa fedha hizo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alimwelekeza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, kwa kushirikiana na madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na wataalamu, kuhakikisha bajeti ya ununuzi na ufungaji wa vifaa vya kinga radi katika shule inaandaliwa na kutekelezwa kupitia bajeti ya Halmashauri.
Mnyeti alisisitiza kuwa shule zinapaswa kuwa sehemu salama kwa wanafunzi na kwamba changamoto zinazoweza kutatuliwa kupitia mipango na bajeti za Serikali zisigeuzwe kuwa mzigo kwa watoto.Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Shule za Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Mercelina Mbehoma, akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa, alieleza kuwa Halmashauri itazingatia na kutekeleza maelekezo yaliyotolewa.
Awali, Diwani wa Kata ya Igulwa, Richard Mabenga, aliiomba Serikali kupitia Ofisi ya Mkoa wa Geita kuangalia uwezekano wa kuufikisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi maeneo ya Bukombe, hususan Ushirombo mjini, katika mipango ya Serikali ya kusambaza maji.
Mabenga alisema Serikali imeendelea kupeleka fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo akaiomba Serikali kuendelea kuangalia mahitaji ya wananchi wa Bukombe, ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema maelekezo ya Mkuu wa Mkoa yatafanyiwa kazi.

Comments
Post a Comment