NELVIN AWASHUKIA VIJANA KUITUMIKIA JUMUIA KWA MISINGI YA MAADILI

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Nelvin Ndugu, amewataka vijana wa jumuiya hiyo katika ngazi za matawi na kata kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, kujituma na kutanguliza masilahi ya chama na jamii badala ya masilahi binafsi.

Wito huo umetolewa wakati wa ziara yake pamoja na Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Wilaya ya Bukombe katika kata za Bugelenga, Iyogelo na Ushirombo, ikiwa ni sehemu ya kutathmini uhai wa chama na jumuiya zake katika maeneo hayo.Katika ziara hiyo, Ndugu alisema amebaini changamoto ya baadhi ya vijana kutanguliza masilahi binafsi katika utekelezaji wa majukumu yao, hali ambayo alisema inaweza kudhoofisha juhudi za kujenga viongozi vijana wenye uzalendo, kujituma na kuwajibika.

“Hatuwezi kuandaa vijana wanaopenda masilahi kila wanapoitwa wanataka posho. Vijana wenzangu, mimi nafanya ziara sina posho wala mshahara. Nawaomba viongozi wangu wa matawi wawajibike na wasimamie vijana wawe wazalendo kwa kujitoa ili kuandaa viongozi bora wasiopenda masilahi binafsi. Hatuwezi kuwa na vijana wanaojitokeza wakati wa uchaguzi tu,” alisema Ndugu.Alisema vijana wanapaswa kuwa na mabadiliko ya fikra katika namna wanavyokihudumia chama, akisisitiza umuhimu wa kujitolea, uzalendo na kutekeleza majukumu waliyopewa bila kutanguliza masilahi binafsi.

Aidha, Ndugu aliwataka vijana kujituma katika shughuli za uzalishaji na kuunda vikundi vya kiuchumi na kuvihakikisha vinasajiliwa ili viweze kunufaika na fursa mbalimbali, ikiwemo mikopo inayotolewa na halmashauri.Pia aliwataka viongozi wa UVCCM katika ngazi za matawi na kata, wakiwemo makatibu, kusimamia kwa karibu utekelezaji wa majukumu katika maeneo yao ili kuhakikisha kila kiongozi na mwanachama anatimiza wajibu wake.

Alisema viongozi hao wanapaswa kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za chama, kuunga mkono jitihada za Serikali, kufanya vikao kwa mujibu wa taratibu na kuhakikisha maamuzi yanayofikiwa yanatekelezwa.

Ndugu pia aliwataka viongozi wa matawi ya UVCCM kufanya vikao na kuwasilisha taarifa katika ngazi husika, huku mabalozi wakitekeleza majukumu yao ya kufanya vikao, kusajili wanachama wapya na kuhamasisha wanachama kulipa ada.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Iyogelo, Mohamed Mdimila, alisema vijana wanapaswa kubadilika, kujituma na kuwajibika katika kutekeleza majukumu yao.Aliwataka wazazi kuendelea kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama na jamii.Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM Tawi la Bugando, Gorige Lukala, alimshukuru Mwenyekiti huyo kwa kuwafikia vijana na kusikiliza changamoto zao, akisema maelekezo yaliyotolewa watayafanyia kazi.Akiwa Kata ya Ushirombo, Ndugu aliwataka vijana kuendelea kuwajibika ndani ya chama, huku akiwataka wanachama wengine kumuunga mkono Diwani wa kata hiyo kwa kushirikiana na Mtendaji wa Kata katika kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.

Comments