MJUE GOLIKIPA BORA WA KNK CUP 2026

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Golikipa Damas Emmanuel Buyenze wa timu ya Ushirombo Warriors FC ametwaa tuzo ya Golikipa Bora wa mashindano ya Kusema na Kutenda (KNK) CUP 2026, baada ya kuisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.Damas alitangazwa kuwa Golikipa Bora na Mratibu wa KNK CUP 2026, Bosco Mwidad, wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa mashindano hayo yaliyofanyika katika Uwanja wa Bukombe Stadium. Katika fainali, Ushirombo Warriors FC ilitwaa ubingwa baada ya kuichapa Katome FC mabao 2-0, huku mabao hayo yakifungwa katika dakika ya 43 ya kipindi cha kwanza na dakika ya 59 ya kipindi cha pili.Damas, ambaye pia ni nahodha wa Ushirombo Warriors FC, alikabidhiwa tuzo yake na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Muragili, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Damas alimshukuru Mungu kwa kumwezesha kufikia hatua hiyo, huku akiwapongeza wachezaji wenzake kwa juhudi walizofanya hadi kufanikiwa kutwaa ubingwa.“Namshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa. Tumekuwa tukishiriki mashindano haya kwa muda mrefu bila kufanikiwa kuchukua ubingwa, lakini mwaka huu tumefanikiwa.Tunaamini huu ni mwanzo na tutaendelea kujituma ili kuchukua ubingwa zaidi,” alisema Damas.

Damas alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa wachezaji, viongozi na benchi la ufundi, akiahidi kuendelea kujituma na kusikiliza maelekezo ya mwalimu wa timu.Kwa mjibu wa Damas Ushirombo Warriors FC ilicheza jumla ya michezo 11, ikashinda michezo 8, huku ikiruhusu mabao 5 na kupata clean sheets tatu hadi kufikia mchezo wa fainali.

Aidha, Damas alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini KNK CUP, akisema mashindano hayo yamekuwa fursa muhimu kwa vijana kuonyesha vipaji vyao na kupata nafasi ya kuonekana zaidi.Katika tuzo nyingine, Maxmilian Revokatus wa Ushirombo Warriors FC alitangazwa kuwa Beki Bora wa KNK CUP 2026, baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika nafasi ya beki wa kushoto.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi, Maxmilian alimshukuru Dkt. Doto Biteko kwa kuanzisha na kuendelea kudhamini mashindano hayo, akisema KNK CUP imekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana katika Wilaya ya Bukombe.

Alisema mashindano hayo yanawapa vijana nafasi ya kuonyesha uwezo wao na kuwafanya waonekane kwa timu kubwa zaidi za soka.Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Muragili, aliwapongeza wachezaji, viongozi na wadau wote walioshiriki KNK CUP 2026, akiwataka timu ambazo hazikufanikiwa kufika fainali kutokata tamaa, bali kuendelea kufanya maandalizi mapema kwa ajili ya mashindano yajayo.KNK CUP 2026 imekuwa sehemu ya mashindano yanayolenga kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha umoja na mshikamano wa wananchi pamoja na kutoa fursa kwa vijana kupitia michezo. 


Comments

  1. Kazi nzuri na jambo hili ni jema .....niwapongeze waandaaji na washiriki na wadau wote mkiwemo nyinyi wanahabari kwa ushiriki mkubwa wenye maslahi mapana ya kukuza vipaji vya vijana wa Bukombe.

    By Diego .......

    ReplyDelete

Post a Comment