MAIGA FOUNDATION-TANZANIA YAKABIDHI MISAADA KWA WAHITAJI BUKOMBE

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Shirika la Maiga Foundation-Tanzania limekabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa makundi yenye uhitaji, ikiwemo wanafunzi wanaohitaji vifaa vya shule, wajane pamoja na watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika katika Kata ya Igulwa, Mlezi wa makundi yanayosaidiwa na Maiga Foundation-Tanzania, Sada Ramadhani, amelipongeza shirika hilo kwa kuendelea kutoa misaada kwa wananchi wenye mahitaji mbalimbali, akisema hatua hiyo ni sehemu ya matendo ya huruma na upendo kwa jamii.Ramadhani amewataka watu wenye uhitaji kuendelea kushirikiana na Maiga Foundation-Tanzania ili waweze kunufaika na huduma na misaada inayotolewa na shirika hilo.

Aidha, amewahimiza walengwa wa misaada hiyo kushirikiana na Serikali kwa kuunda vikundi vya wajasiriamali, ili waweze kuomba mikopo isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri kwa ajili ya kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuboresha maisha ya familia zao.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Maiga Foundation-Tanzania Wilaya ya Bukombe, Frank Kaare, amesema shirika hilo limeanza kwa kuangalia mahitaji ya makundi mbalimbali, hasa watoto yatima na wanafunzi, ambao wamekuwa wakisaidiwa vifaa vya shule.

Amesema pia wajane na watu wenye ulemavu wamepokea misaada mbalimbali, ikiwemo sabuni, miche pamoja na unga, kulingana na mahitaji yao.

Kaare amesema makundi hayo bado yana mahitaji mengi na kwamba baadhi yao wamekuwa wakijihusisha na shughuli za ujasiriamali, ikiwemo kilimo cha bustani za mboga mboga na ufugaji, hivyo wana uwezo wa kunufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri ili kukuza shughuli zao.Ameziomba taasisi na wadau mbalimbali kuendelea kuyashika mkono makundi yenye uhitaji, huku akiwapongeza madiwani, Mbunge wa Jimbo la Bukombe Dkt. Doto Biteko, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe kwa ushirikiano wanaoupa uongozi wa Maiga Foundation-Tanzania pale wanapohitaji huduma na ushirikiano.

Mmoja wa walengwa wa msaada huo, Christina Gerard, ameliomba shirika hilo kuendelea kuwasaidia hasa wajane, akisema misaada waliyoipokea itawasaidia kukabiliana na mahitaji ya familia.Christina amesema wanafunzi waliopatiwa madaftari wamepata msaada mkubwa katika kuendelea na masomo yao, huku akiwashukuru Maiga Foundation-Tanzania na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kutoa misaada kwa watu wenye mahitaji.

Naye Elia Sagata, kwa niaba ya watu wenye ulemavu na wenye mahitaji maalumu, amelishukuru Maiga Foundation-Tanzania kwa misaada iliyotolewa, akisema imekuwa na umuhimu mkubwa kwa walengwa.Sagata amewaomba wadau mbalimbali kuendelea kuwasaidia watu wenye ulemavu na mahitaji maalumu, ikiwemo kuwawezesha kupata mikopo inayotolewa na Halmashauri ili waweze kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwinjilisti Esau Marifedha amelipongeza Maiga Foundation-Tanzania kwa kutoa msaada huo, akisema ni ishara ya upendo, huruma na uwajibikaji kwa jamii.Amesisitiza umuhimu wa shirika hilo kuendelea kuwafikia watu wenye uhitaji katika maeneo mbalimbali ili kuwasaidia kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao.

Comments