Matumizi ya gesi asilia nchini Tanzania yametajwa kuongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni, huku Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ikisisitiza umuhimu wa kuendelea kuielimisha jamii kuhusu matumizi, faida na mchango wa nishati hiyo katika maendeleo ya taifa.
TPDC imekutana na wanahabari kwa nyakati tofauti wa mikoa nane inayopitiwa na mradi wa bomba la mafuta ghafi la Africa Mashariki kutoka Uganda hadi Tanga Tanzania na kuwataka kutumia nafasi yao kuwaelimisha wananchi.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TPDC , Marie Msellemu amesema, wanahabari wanayo nafasi kubwa kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa gesi asilia na fursa zinazotokana na matumizi ya nishati hiyo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uelewa wa jamii kuhusu nishati safi na salama.
Msellemu amefafanua kuwa, gesi asilia imeendelea kutumika katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo uzalishaji wa umeme, viwanda, usafirishaji pamoja na matumizi ya majumbani.
Kuongezeka kwa matumizi hayo kunaelezwa kuwa ni sehemu ya mabadiliko katika sekta ya nishati, huku serikali ikilenga kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata fursa ya kutumia nishati hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka TPDC, kwa sasa zaidi ya wateja 2,000 nchini wanatumia gesi asilia, huku mkoani Mtwara pekee zaidi ya kaya 1,000 zikiwa zimeunganishiwa nishati hiyo.
Hali hiyo inaonyesha namna matumizi ya gesi asilia yanavyozidi kupanuka kutoka katika matumizi ya viwandani na uzalishaji wa umeme hadi kuwafikia wananchi katika matumizi ya kila siku.Mbali na matumizi ya viwandani na majumbani, gesi asilia imeanza pia kupata nafasi katika sekta ya usafirishaji.
TPDC imeeleza kuwa zaidi ya magari 20,000 nchini yanatumia gesi asilia, hali inayodhihirisha kuwa nishati hiyo imeanza kuwa sehemu ya muhimu katika sekta ya usafiri.
Miongoni mwa watumiaji wa gesi asilia katika magari ni Kampuni ya Dangote, ambayo ni moja ya kampuni zinazotumia nishati hiyo katika shughuli zake.
Aidha, matumizi ya gesi asilia kwenye magari yanaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa baadhi ya nishati zinazotokana na mafuta ya petroli, huku pia yakichangia katika juhudi za kupunguza matumizi ya nishati zinazoweza kuongeza uchafuzi wa mazingira.
Kwa mujibu wa Msellemu, viwanda vinavyotumia gesi asilia vinachangia asilimia 20 ya matumizi ya gesi hiyo, wakati asilimia 80 inatumika katika mitambo ya kuzalisha umeme.
Takwimu hizo zinaonyesha nafasi kubwa ambayo gesi asilia imekuwa nayo katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme nchini, hasa wakati Tanzania ikiendelea kupanua shughuli za uzalishaji na matumizi ya umeme kwa wananchi na sekta mbalimbali za uchumi.
Katika kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kutumia gesi asilia, TPDC imeendelea na jitihada za kuunganisha kaya katika maeneo mbalimbali nchini.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa nyumba 1,984 zilizopo katika maeneo ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Kisemvule zimeunganishiwa nishati hiyo.
Msellemu amesema, lengo la Serikali ni kuhakikisha gesi asilia inawafikia wananchi wengi zaidi nchini, ikiwa ni sehemu ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kupunguza utegemezi wa nishati chafu.
Kwa mtazamo huo, ongezeko la matumizi ya gesi asilia linaweza kuwa sehemu ya mpito kuelekea matumizi makubwa zaidi ya nishati zenye athari ndogo kwa mazingira.
“iIi wananchi waweze kutumia nishati hiyo kwa kiwango kikubwa zaidi, uelewa wa jamii ni jambo muhimu. Ndiyo maana TPDC imewataka wanahabari kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu kwa umma kuhusu gesi asilia”, amesema Msellemu.
Hata hivyo, wakati matumizi ya gesi asilia yakizidi kuongezeka, Tanzania pia inaendelea kutekeleza miradi mikubwa katika sekta ya mafuta, ikiwemo mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanga, unaojulikana kama EACOP.
Mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta ya nishati inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda.
Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Kaimu Mratibu wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanga (EACOP) kutoka TPDC, Jumanne Mohamed Said, amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 87.8.
Said amesema mradi huo unatarajiwa kuanza kufanya kazi Januari 15, 2027.Kwa mujibu wa maelezo yake, bomba hilo litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 ya mafuta ghafi kwa siku.
Hii ina maana kuwa baada ya kukamilika na kuanza kufanya kazi, bomba hilo litakuwa na uwezo mkubwa wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga, ambako mafuta hayo yataweza kusafirishwa kwenda kwenye masoko mbalimbali.Mradi wa EACOP unahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilomita 1,443.
Kati ya umbali huo, kilomita 1,147 ni sehemu ya njia inayopita nchini Tanzania kutoka Kagera hadi Tanga.
Ujenzi wa bomba hilo unaifanya Tanzania kuwa sehemu muhimu katika miundombinu ya usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Uganda kuelekea katika soko la kimataifa kupitia bandari ya Tanga.
Kwa Tanzania, mradi huo una umuhimu katika sekta ya nishati, usafirishaji na uchumi kwa ujumla, huku pia ukihusisha uwekezaji mkubwa na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika maeneo ambayo bomba hilo linapita.
Mikoa inayopitiwa na mradi huo wa Bomba la Mafuta EACOP ni pamoja na Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara, Dodoma na Tanga, na katika mradi huo, Tanzania ina ubia wa asilimia 15.
Ushiriki huo unaifanya Tanzania kuwa mshirika muhimu katika mradi wa EACOP na kuweka nafasi ya nchi kunufaika na shughuli zinazohusiana na mradi huo kwa mujibu wa mikataba na taratibu zilizowekwa.
Kwa upande mwingine, Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi ya mafuta na gesi inawanufaisha Watanzania kupitia ajira, biashara, uwekezaji, ujuzi na mapato kwa taifa.
Baadhi ya waandishi wa habari waliofikiwa na elimu hiyo miradi hiyo ya nishati wamesema ni hatua nzuri ya serikali katika kuhakikisha wananchi wanafikiwa na nishati hiyo.
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita (GPC) Renatus Masuguliko amesema, baadhi ya wana habari katika mkoa huo hawakuwa na elimu kuhusu TPDC na Bomba la mafuta la AfriKa Mashariki ECOP.
“Tumefurahishwa na mafunzo ya elimu hii ,kwani mmetujengea uelewa mpana mno miongoni mwetu ,na ndiyo maana mmejionea wenyewe wanahabari wa Geita wamekuwa na shauku kubwa ya kuuliza maswali mengi lengo ni kujifunza zaidi” amesema Masuguliko.

Comments
Post a Comment