WAZAZI WATAKIWA KUWALEA WATOTO KIMAADILI ILI KUWA VIONGOZI BORA


Na Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Wazazi na walezi nchini wametakiwa kuwalea watoto wao kwa kuzingatia maadili mema ya Kitanzania na kuwapa elimu bora ili wakue na kuwa viongozi bora wa taifa, kanisa na jamii.

Wito huo umetolewa na Makamu Askofu Mkuu wa Muunganiko wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (MMPT), Wilson Balayata, wakati wa ibada ya uzinduzi wa Misheni ya Ushirombo na kusimikwa kwa viongozi wa misheni hiyo mjini Ushirombo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.

Balayata alisema wazazi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya heshima, unyenyekevu, utii na uwajibikaji.

Alisema vijana wanapaswa kuwasikiliza wazazi wao na kuheshimu malezi wanayopewa, kwa kuwa misingi hiyo inaweza kuwaandaa kuwa viongozi bora katika kanisa, Serikali na jamii.

Aidha, aliwataka watumishi wa Mungu kuendelea kuwa wanyenyekevu na kuheshimu viongozi pamoja na mamlaka za juu, akisema Mungu huweza kumuinua mtu anayekuwa mwaminifu katika huduma.Baada ya kusimikwa kuwa Makamu Askofu wa Misheni ya Ushirombo, Juma Ezekiel Mathias, alisema safari yake ya huduma ilianza katika familia ya Kiislamu, kabla ya kuokoka na kujiunga na kanisa.

Mathias alisema alizaliwa mwaka 1970, mwaka 1975 akaokoka na mwaka 1977 akajiunga na kanisa hilo.Alisema alianza kuhudumu kanisani kama mwimbaji wa Sande, baadaye akajiunga na kwaya na kuwa mwenyekiti wa Goligotha Kwaya.

Mwaka 2011 alihitimu chuo cha Biblia na kuwa mchungaji wa tawi la Uinjilisti, huku mwaka 2013 akibarikiwa kuwa mchungaji wa Parishi ya Ushirombo.

Mathias aliwashukuru Makamu Askofu Mkuu Wilson Balayata na Askofu Mkuu wa MMPT Tanzania, Elieza Mazinge, kwa kuipandisha hadhi Parishi ya Ushirombo kuwa Misheni na kumuinua kuwa Makamu Askofu.

Aliahidi kushirikiana na waumini pamoja na viongozi wake wa juu, akiwemo Askofu wa Misheni ya Ushirombo, MMPT Kalebu Buluma, katika kuimarisha huduma ya kanisa.Muumini wa MMPT, Savera Mugisha, aliushukuru uongozi wa kanisa kwa kuipandisha hadhi Parishi ya Ushirombo kuwa Misheni, akisema hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa huduma za kiroho kwa waumini.

Naye Anthony Evarist alisema waumini wamefurahia kuwa na viongozi wa ngazi ya Maaskofu katika Misheni hiyo, kwa kuwa huduma ambazo hapo awali walizifuata maeneo ya mbali sasa zitapatikana Ushirombo.

Katibu wa Kanisa la Pentekoste Ushirombo, Paskali Kantu, akisoma taarifa ya kanisa, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa kazi ya kuleta miradi ya maendeleo katika Jimbo la Bukombe.

Kantu pia aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha na kulinda amani ya Tanzania.Alisema kanisa litaendelea kuiombea Serikali pamoja na viongozi wake ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya wananchi.Katika taarifa hiyo, Kantu alisema kanisa linakabiliwa na changamoto ya kukamilisha ujenzi wa kanisa la Misheni ya Ushirombo.Alisema waumini na wahisani mbalimbali tayari wamechangia jumla ya Shilingi milioni 36,575,800, huku boma la kanisa likiwa limekamilika.

Alisema kanisa linahitaji Shilingi milioni 159,250,000 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi, ikiwemo hatua ya kuezeka inayokadiriwa kugharimu takribani Shilingi milioni 100.

Mahitaji yaliyobaki ni pamoja na bati bado 64 za msauzi, vyuma vya kechi 3,500, papi 150 na misumari yenye uzito wa kilo 80.

Katika harambee hiyo, Diwani wa Kata ya Katente, Kasuluzu Ng’hwani, alichangia Shilingi 200,000, huku Diwani wa Kata ya Bugelega, Donald Lubigisa, akichangia bati 10 na kuahidi kuifikisha taarifa hiyo kwa viongozi wengine ili nao waweze kushiriki katika ujenzi wa kanisa hilo.

 

Comments