Na, Ernest Magashi
Umoja wa Utamaduni wa Watu wa Mapacha Kanda ya Magharibi, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, umepewa elimu kuhusu namna ya kunufaika na mikopo isiyo na riba inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri, ikiwemo mikopo ya fedha na pikipiki kwa vikundi vinavyokidhi vigezo.
Elimu hiyo ilitolewa na Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Bukombe, Gerevas Nkononziku, wakati wa hafla ya kutangaza Katiba ya Kanda ya Magharibi ya Kikundi cha Kiutamaduni cha Watu wa Mapacha, iliyofanyika katika Kijiji cha Mtinga, Kata ya Ng'anzo, Wilaya ya Bukombe.
Nkononziku alisema wanachama wa umoja huo wanapaswa kuunda vikundi vya wanawake, vijana au watu wenye ulemavu vyenye angalau wanachama watano, kisha kuvisajili kuanzia ngazi ya kata ili vipate sifa ya kunufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri.
Alisema hatua hiyo itasaidia wanamapacha kupata mtaji wa kuendesha shughuli zao na kupunguza utegemezi wa michango ya mara kwa mara wanapokuwa na shughuli za kijamii na kiutamaduni.
Awali, Katibu wa Utamaduni wa Watu wa Mapacha Kanda ya Magharibi, Seselo Dangamila, akisoma taarifa ya umoja huo alisema utamaduni wa asili ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa na unapaswa kulindwa, kuenziwa na kuendelezwa.
Dangamila alisema kwa sasa umoja huo unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha za kuendesha shughuli zake, hali inayowalazimu wanachama kuchangishana fedha kutoka mifukoni mwao.
"Tunaiomba Serikali itusaidie na kutuwezesha kwa namna itakavyoona inafaa ili kuimarisha mfuko wetu wa wanamapacha. Hii itapunguza utegemezi wa michango na kutusaidia kuendesha shughuli zetu kwa ufanisi zaidi," alisema Dangamila.
Akitoa salamu za Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Afisa Michezo wa Wilaya ya Bukombe, Jenipha Kisus, aliwahamasisha wanachama wa umoja huo kuendelea kuenzi utamaduni wa Kitanzania na kuwalea watoto katika misingi ya maadili mema.
Pia aliwataka wanachama kuanza kuweka akiba na kujijengea utamaduni wa kuchangia mfuko wa kikundi ili iwe rahisi kukidhi masharti ya kupata mikopo ya Halmashauri na kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Naye Diwani wa Kata ya Ng'anzo, Mashaka Shing'wenda, alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kutekeleza ombi lao la kusaidia shughuli za wanamapacha, huku akiwahimiza wanachama kutumia fursa za mikopo isiyo na riba kujikwamua kiuchumi na kuimarisha umoja wao.

Comments
Post a Comment