Na, Ernest Magashi
Wanachama wa Shirika la Itumikie Tanzania, Nchi Yako (INYATA) wametakiwa kuendelea kuwa mabalozi wa amani, upendo, umoja na uzalendo kwa kuitangaza na kuitetea amani ya Tanzania katika jamii.
Wametakiwa pia kutoa elimu kwa wananchi, hususan vijana, kuhusu umuhimu wa kulinda amani, kuheshimu maadili na kuwajibika katika maeneo yao ili kujenga jamii yenye mshikamano na utulivu.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa INYATA Mkoa wa Geita, John Alphonce Sumuni, wakati akitoa mwongozo wa utendaji kazi kwa viongozi wa wilaya za Mkoa wa Geita katika kikao kilichofanyika Wilaya ya Bukombe.
Sumuni amesema viongozi wa INYATA wanapaswa kuusoma na kuuelewa mwongozo wa utendaji kazi ili kutambua majukumu yao na kuyatekeleza kwa kujituma, huku wakitoa mchango wao katika kuijenga jamii yenye maadili na uzalendo.
Amesema vijana ni sehemu muhimu katika kulinda amani ya nchi, hivyo INYATA ina wajibu wa kuwafikia na kuwapa elimu itakayowasaidia kutambua thamani ya amani na utulivu wa Tanzania.
“Wawe wazalendo wa kweli na tuwajibike katika maeneo yetu tunayoishi ili jamii iwe na maadili safi. Tuendeleze utulivu na mshikamano wa taifa letu,” alisema Sununi.
Sumuni amesema INYATA Mkoa wa Geita hivi karibuni itaanza kufanya ziara za kimkakati katika wilaya mbalimbali kwa lengo la kukutana na wanachama, kuwapa mwongozo na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo.
Amesisitiza kuwa INYATA si shirika la kisiasa wala la Serikali, bali limeanzishwa na Watanzania kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa amani, upendo, uzalendo na mshikamano wa kitaifa.
Amewataka viongozi wa wilaya kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi kwa upana zaidi, ili kila mmoja aweze kutambua wajibu wake katika kulinda amani na misingi ya taifa.
Aidha, Sumuni amepongeza uongozi wa INYATA Wilaya ya Bukombe kwa kujituma na kujiandaa katika utekelezaji wa majukumu yake, akisema juhudi hizo zinapaswa kuendelezwa ili ujumbe wa INYATA ufike kwa wananchi wengi zaidi.
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya INYATA Wilaya ya Bukombe, Agnes Msomi, amewataka viongozi na wanachama kuwa na ushirikiano katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.Msomi amesema mshikamano na ushirikiano ni muhimu katika kuhakikisha INYATA inaendelea kutoa elimu kwa jamii kwa ufanisi.
Naye Mjumbe wa INYATA Mkoa wa Geita, Stela Simbila, amewashukuru viongozi wa mkoa kwa kufika Bukombe na kuendelea kutoa elimu kuhusu misingi na malengo ya shirika hilo.Simbila amesema ataendelea kutekeleza majukumu yake ya kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa amani, upendo, uzalendo na mshikamano.
Kwa upande wake, Katibu wa Hamasa wa INYATA Wilaya ya Bukombe, Isaya Paul, amewashukuru viongozi wa mkoa kwa ujio wao, akisema kikao hicho kimemsaidia kupata maarifa na mwongozo utakaomsaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Katibu wa INYATA Wilaya ya Bukombe, Dida Kisika, amesema uongozi wa wilaya utahakikisha unatekeleza maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa INYATA Mkoa wa Geita ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Mwenyekiti wa INYATA Wilaya ya Bukombe, Joseph Mponzemenya, amewashukuru viongozi wa Mkoa wa Geita kwa kuchagua kufanya kikao hicho katika Wilaya ya Bukombe, akisema kimekuwa na manufaa makubwa kwa viongozi na wanachama.
Mponzemenya amesema kupitia kikao hicho wamepata elimu na maelekezo muhimu yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Ameahidi kuwa uongozi wa INYATA Wilaya ya Bukombe utaendelea kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa, huku akiwataka wanachama kuendelea kuwa na mshikamano, ushirikiano na kujituma ili kufikia malengo ya shirika.
Kwa ujumla, viongozi wa INYATA wameendelea kusisitiza umuhimu wa jamii kushiriki katika kulinda amani, kudumisha upendo na mshikamano, pamoja na kujenga kizazi chenye uzalendo na kuheshimu misingi ya taifa.

Comments
Post a Comment