VIJANA CHANGAMKIENI FURSA ZA MIKOPO YA HALMASHAURI

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Vijana wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wametakiwa kuchangamkia fursa za mikopo isiyo na riba ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, kwa kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.Wito huo umetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Bukombe, Melania Kwai, wakati akizungumza katika Kongamano la Vijana Platform lililofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, likiwa na lengo la kuwajengea vijana uelewa, kuwaibulia fursa mbalimbali na kuhamasisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo ya jamii na kukuza uchumi wao pamoja na Taifa kwa ujumla.

Kwai amesema vijana wana nafasi kubwa ya kunufaika na mikopo hiyo, hivyo amewataka kuunda vikundi na kuvisajili kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kata zao, kisha kuwasilisha maombi ya mikopo yakiambatana na andiko la mradi wanaokusudia kuufanya kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.Amesema Halmashauri inatoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo kiasi cha mikopo kinachotolewa huanzia shilingi milioni tano hadi milioni 150, kulingana na mahitaji na uwezo wa kikundi pamoja na taratibu za mikopo.Kwai amevitaka vikundi vinavyopatiwa mikopo kuhakikisha vinatumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati kwa mujibu wa masharti ya mikopo, ili kuepuka kuwa wadaiwa sugu na kuchukuliwa hatua za kisheria.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, amewahimiza vijana kuchangamkia fursa za mikopo hiyo, akisema ni miongoni mwa njia muhimu zinazolenga kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi, kuanzisha na kukuza shughuli za uzalishaji.Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, amesema Kongamano la Vijana Platform ni msukumo mpya kwa vijana, unaolenga kuwajengea uwezo wa kufikiri kwa ubunifu, kutumia fursa zilizopo na kujenga msingi wa kujitegemea kiuchumi.

Akifunga kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, amesema Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya vikundi au wanachama watakaoshindwa kurejesha mikopo kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa.Mhandisi Muragili amesema Serikali inaendelea kutambua vijana kama nguvu kazi muhimu ya Taifa na itaendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha kutumia nguvu na ubunifu wao katika kujiletea maendeleo.

“Vijana msiishie kusikiliza elimu mnayopewa hapa, bali hakikisheni mnayafanyia kazi kwa vitendo ili iwe chachu ya mabadiliko na maendeleo katika maisha yenu,” amesema Mhandisi Muragili.Aidha, amesema vijana ni chachu ya maendeleo ya nchi, hususan katika sekta ya uchumi, hivyo wanapaswa kujitambua, kutumia fursa zilizopo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.

Amesema vijana wana nafasi kubwa ya kuwa na maono, ubunifu na nguvu kazi inayoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Taifa, hivyo wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kwa manufaa yao, jamii na nchi kwa ujumla.

Comments