USHIROMBO WARRIORS YATWAA UBINGWA WA TARAFA YA USHIROMBO KNK CUP 2026


Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Timu ya Ushirombo Warriors imetwaa ubingwa wa Tarafa ya Ushirombo katika mashindano ya KNK CUP 2026, baada ya kuichapa Wolves FC mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Ushirombo.

Ushirombo Warriors ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 28 kupitia mshambuliaji Igayo Igayo, aliyefanikiwa kuandika bao hilo na kuipa timu yake matumaini ya kutwaa ubingwa.Wolves FC, inayotokea Kata ya Igulwa, ilirejea kipindi cha pili ikiwa na nguvu na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 69 kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na mshambuliaji Mudi Kayombo, baada ya kuchezewa madhambi ndani ya eneo la hatariHata hivyo, Ushirombo Warriors haikukubali presha hiyo na dakika ya 73 ilipata bao la pili kupitia mshambuliaji wake Mboma Majeshi, aliyefanikiwa kuupenya ulinzi wa Wolves FC na kuipa timu yake ushindi wa mabao 2-1 hadi filimbi ya mwisho.

Baada ya mchezo huo, nahodha wa Ushirombo Warriors, Damas Buyenze, alianza kwa kumshukuru Mungu pamoja na wachezaji wenzake, akisema ushindani ulikuwa mkubwa lakini wamepambana hadi kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Tarafa ya Ushirombo.Buyenze alisema timu hiyo sasa inaweka nguvu katika maandalizi ya hatua inayofuata ya mashindano hayo, ikiwa na lengo la kuwania ubingwa wa Wilaya ya Bukombe.

Aidha, nahodha huyo alimpongeza mdhamini wa KNK CUP 2026 na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano hayo, akisema yamekuwa chachu ya kuibua na kukuza vipaji vya vijana katika michezo.

Kwa upande wake, nahodha wa Wolves FC, Musa Charles, alisema wamepokea matokeo hayo kwa moyo wa kiungwana, huku akimshukuru Mungu na wachezaji wenzake kwa kujituma katika mchezo huo.“Wachezaji wamejituma uwanjani, lakini leo haikuwa siku yetu. Tumefanya makosa na tumeadhibiwa,” alisema Charles.Akikabidhi zawadi kwa bingwa na mshindi wa pili, Mratibu wa KNK CUP 2026 Wikaya ya Bukombe , Bosco Mwidadi, alisema mashindano hayo yanadhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa lengo la kuwaunganisha wananchi pamoja na kuibua vipaji kwa vijana.Kwa kutwaa ubingwa huo, Ushirombo Warriors imejinyakulia Shilingi 300,000 pamoja na mpira mmoja, huku mshindi wa pili, Wolves FC, akipewa Shilingi 100,000 pamoja na mpira mmoja.

Comments