Timu mbili zimefanikiwa kutanguliza mguu kuelekea fainali ya mashindano ya KNK CUP 2026 ngazi ya Tarafa, yanayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, Dkt. Doto Biteko, baada ya kuibuka na ushindi katika michezo ya hatua ya nusu fainali.
Katika michezo iliyochezwa jana, Ng’anzo FC iliibuka na ushindi wa mabao 8-7 dhidi ya Butinzya FC, matokeo yaliyoifanya Butinzya FC kuondolewa katika mashindano hayo, huku Ng’anzo FC ikisonga mbele kuelekea fainali.
Katika mchezo mwingine, Lane Academy FC iliibuka na ushindi wa bao 1-1 dhidi ya Napalahala FC, na hivyo kuiondoa Napalahala FC kwenye mashindano kwa kukeuka kanuni za mashindano hayo na kuiwezesha Lane Academy FC kutanguliza mguu kuelekea fainali.
Akizungumza na Bukombe Sasa Media kuhusu hatua ya mashindano hayo, Katibu wa KNK CUP, Domician Kabalenga, amesema michuano hiyo imeendelea kwa ushindani mkubwa huku timu zikisaka nafasi ya kutwaa ubingwa wa ngazi ya Tarafa.
Kabalenga amesema jumla ya timu 248 zilisajiliwa na kuanza kinyang’anyiro hicho tangu Julai 1, 2026, ambapo baada ya michezo ya mtoano, timu 17 zimefanikiwa kufuzu na kutwaa ubingwa katika ngazi ya Kata, huku timu 231 zikishindwa kufuzu na kuondolewa kwenye mashindano.
Amesema kwa sasa mashindano yameingia katika hatua ya kuzikutanisha timu zilizofanya vizuri katika ngazi ya Kata, ambazo zinapambana kuwania ubingwa wa Tarafa kabla ya mshindi kusonga mbele katika hatua inayofuata.
“Zawadi kwa timu itakayofanikiwa kutwaa ubingwa wa Tarafa zipo tayari, na tunatarajia mashindano yataendelea kuwa na ushindani mkubwa hadi kupata bingwa,” alisema Kabalenga.
Mashindano ya KNK CUP 2026 yanafanyika katika tarafa za kimichezo za Siloka, Bukombe, Ushirombo, Ng’anzo na Bulenga, ambapo timu zinapambana kuwania ubingwa katika hatua mbalimbali za mashindano hayo.

Comments
Post a Comment