Rais wa Utamaduni wa Watu wa Mapacha Kanda ya Magharibi, Shirugu Lubigisa, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kushirikiana na wazazi wa watoto mapacha pamoja na kuwapatia zawadi kama ishara ya kuthamini na kuenzi utamaduni wao.
Lubigisa alitoa pongezi hizo wakati wa hafla ya kutangaza Katiba ya Kanda ya Ziwa Magharibi ya Kikundi cha Kiutamaduni cha Watu wa Mapacha, iliyofanyika katika Kijiji cha Mtinga, Kata ya Ng'anzo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Alisema Dkt. Biteko ni kiongozi mwenye moyo wa kujali wananchi na anastahili kupongezwa kwa mchango wake katika kuimarisha ustawi wa jamii. Alieleza kuwa, mbali na kuwasaidia wazazi wa mapacha, Dkt. Biteko ameendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imebadilisha sura ya Wilaya ya Bukombe, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu.
Katibu wa Utamaduni wa Watu wa Mapacha Kanda ya Magharibi, Seselo Dangamila, akisoma taarifa ya umoja huo alisema utamaduni wa asili ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote na unapaswa kulindwa na kuenziwa.
Kwa upande wake, Lubigisa alisema maendeleo hayawezi kupatikana kwa kuiga tamaduni za kigeni zinazokwenda kinyume na maadili ya Kitanzania. Alibainisha kuwa baadhi ya tamaduni hizo huchangia mmomonyoko wa maadili kwa vijana na kusababisha migogoro katika jamii, jambo linaloweza kudhoofisha maendeleo ya taifa.
Akitoa salamu za Mbunge Dkt. Doto Biteko, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Afisa Michezo wa Wilaya ya Bukombe, Jenipha Kisus, aliwahamasisha wanachama wa umoja wa mapacha kuendelea kuenzi utamaduni wa Kitanzania na kuwalea watoto katika misingi ya maadili mema
Kisus pia alikabidhi zawadi zilizotolewa na Dkt. Biteko kwa wazazi wa mapacha na kuwashukuru kwa umoja wao. Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kupitia programu mbalimbali, ikiwemo utoaji wa elimu ya kukuza uchumi wa familia.
Naye Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Bukombe, Gerevas Nkononziku, aliwahimiza wanachama wa umoja huo kuanzisha vikundi vya kiuchumi ili waweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Diwani wa Kata ya Ng'anzo, Mashaka Shing'wenda, alimshukuru Dkt. Doto Biteko kwa kuendelea kushirikiana na wazazi wa mapacha na kuwapatia zawadi. Aidha, aliwahimiza wanachama wa umoja huo kudumisha mshikamano na kutumia fursa ya mikopo isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri kwa ajili ya kuinua uchumi wao, akisisitiza kuwa fedha hizo zinapatikana.

Comments
Post a Comment