MIKWAJU YA PENALTI YAIPELEKA USHIROMBO WARRIORS MBELE, YAICHAPA KATENTE STAR 4–2 KNK CUP 2026

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Timu ya Ushirombo Warriors imefanikiwa kusonga mbele katika mashindano ya KNK Cup 2026 baada ya kuichapa Katente Star kwa mikwaju ya penalti 4–2, kufuatia mchezo wa kusisimua uliowakutanisha mabingwa wa Kata ya Bulangwa na Katente katika hatua ya kusaka ubingwa wa Tarafa ya Ushirombo.Mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Katente ulianza kwa kasi, huku Ushirombo Warriors wakionyesha dhamira ya kutafuta ushindi. Dakika ya 43, Igayo Keneth aliifungia Ushirombo Warriors bao la kwanza, na timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1–0.Kipindi cha pili, Katente Star walirejea uwanjani kwa kasi kubwa na kuongeza mashambulizi langoni mwa Ushirombo Warriors. Juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 67, ambapo Erick Deko alisawazisha na kufanya mchezo kuwa 1–1.Dakika 90 zilimalizika kwa sare ya bao 1–1, hivyo mshindi kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, ambapo Ushirombo Warriors walikuwa makini zaidi na kushinda kwa 4–2, na hivyo kujikatia tiketi ya kusonga mbele katika hatua inayofuata ya mashindano.

Akizungumza baada ya mchezo, Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Bulangwa na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, Peter Mkina, aliwapongeza wachezaji pamoja na benchi la ufundi la Ushirombo Warriors kwa kujituma na kupambana hadi kupata matokeo yaliyowawezesha kusonga mbele.

Mkina alisema ushindi huo ni wa kishindo kwa timu hiyo, huku akieleza kuwa wachezaji wameonyesha moyo wa kupambana na kuwapa mashabiki burudani ya soka.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Katente, David Jeremia, aliwapongeza wachezaji na benchi la ufundi la Katente Star kwa kupambana hadi dakika za mwisho, akiwataka kutokata tamaa na badala yake kuendelea kujipanga kwa msimu ujao.

Jeremia pia alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya KNK Cup 2026, akisema mashindano hayo yamekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa jamii na kutoa burudani kwa wananchi wa Bukombe na maeneo jirani.Ushindi huo unaiweka Ushirombo Warriors katika hatua inayofuata huku ikisubiriwa kwa hamu safari yao ya kusaka ubingwa wa Tarafa ya Ushirombo

Comments