Na, Ernest Magashi
Wanachama na mashabiki wa Yanga SC wilayani Bukombe mkoani Geita wameeleza kufurahishwa na kitendo cha Rais wa Yanga SC, Eng. Hersi Ally Said, kumkabidhi Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, jezi rasmi ya klabu hiyo itakayotumika katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2026/27.
Akizungumza katika shamrashamra za joto la kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara zilizofanyika Bukombe Stadium, mjini Ushirombo, shabiki wa Yanga SC, Lameck Mashauri, alisema tukio hilo ni heshima kubwa kwa wananchi wa Bukombe na linaonyesha namna uongozi wa Yanga SC unavyothamini mchango wa Dkt. Biteko katika maendeleo ya michezo.
Alisema Dkt. Biteko ameendelea kuifanya Bukombe kuwa kitovu cha michezo kwa kufanikisha ujenzi wa Bukombe Stadium, jambo lililowezesha Yanga SC kufika wilayani humo kufanya mazoezi na kukutana na mashabiki wake.
"Tunampongeza Rais wa Yanga SC, Eng. Hersi Ally Said, kwa upendo aliouonyesha kwa kumkabidhi Mbunge wetu, Dkt. Doto Biteko, jezi rasmi ya Yanga SC ya msimu wa 2026/27. Hii ni heshima kubwa kwa Bukombe na inaonyesha ushirikiano mzuri kati ya klabu yetu na viongozi wanaoendeleza michezo," alisema Lameck.
Naye mkazi wa Ushirombo, Lukas Paschal, alisema hakuwahi kufikiria kuwa siku moja angewaona wachezaji wa Yanga SC wakifanya mazoezi katika ardhi ya Bukombe.
Alisema ujio wa Yanga SC pamoja na kitendo cha Rais wa klabu hiyo kumkabidhi Dkt. Biteko jezi mpya ya msimu ni kumbukumbu muhimu kwa mashabiki wa soka wilayani Bukombe na ishara ya kuendelea kukua kwa sekta ya michezo katika eneo hilo.
Klabu ya Yanga imetambulisha mlinzi wa kati Farouk Komara raia wa Nchini Ivory Cost mwenye umri wa miaka 25 aliyekuwa akiichezea timu ya Golden Arrows.

Comments
Post a Comment