MASHABIKI NA WANANCHI WAUNGANA KUSHUHUDIA MAZOEZI YA YANGA SC BUKOMBE STADIUM

Na, Ernest Magashi 

ebukombesasablogspot.com.tz

Wanachama na mashabiki wa Yanga SC, pamoja na mamia ya wananchi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita na maeneo jirani, wamejitokeza kwa wingi kushuhudia mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika katika Uwanja wa Bukombe Stadium, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2026/27.Mashabiki hao walionyesha furaha kubwa kwa kupata nafasi ya kuwaona wachezaji wa Yanga SC wakifanya mazoezi katika uwanja huo wa kisasa uliojengwa mtaa wa Kilimahewa, mjini Ushirombo, Kata ya Katente, Wilaya ya Bukombe.Akizungumza uwanjani hapo, shabiki wa Yanga SC, James Nkamba maarufu kama G'wanankamba, alimshukuru na kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, Serikali pamoja na wadau wa michezo kwa kufanikisha ujenzi wa uwanja huo wa kisasa.Alisema ni jambo la kihistoria kwa wananchi wa Bukombe kushuhudia timu kubwa kama Yanga SC ikifanya mazoezi katika uwanja huo."Nina furaha sana. Hii ni mara ya kwanza kuona Yanga SC wakifanya mazoezi Bukombe Stadium. Tunampongeza sana Dkt. Doto Biteko kwa kuibadilisha Bukombe na kuifanya kuwa kitovu cha matukio makubwa ya michezo na kijamii. Tunaamini hii si mara ya mwisho kuona Yanga SC wakifika hapa," alisema G'wanankamba.Nye shabiki mwingine wa Yanga SC, Pili Jacob, alisema tangu aanze kuishabikia klabu hiyo hajawahi kupata nafasi ya kuwaona wachezaji wa timu hiyo kwa ukaribu kama alivyopata katika mazoezi hayo.Alisema maendeleo yanayoletwa na Dkt. Doto Biteko kwa kushirikiana na Serikali yamewawezesha wananchi wa Bukombe kutimiza ndoto ya kuwaona nyota wa Yanga SC wakifanya mazoezi katika uwanja wa nyumbani."Nimefurahi sana kuwaona kwa macho yangu mastaa wa Yanga SC akiwemo Okello pamoja na wachezaji wengine wakifanya mazoezi. Hii ni fahari kubwa kwetu mashabiki wa Bukombe," alisema.Katika hafla hiyo, Rais wa Yanga SC, Eng. Hersi Ally Said, alimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, jezi rasmi ya klabu hiyo itakayotumika katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2026/27 kama ishara ya kuthamini mchango wake katika maendeleo ya michezo.Akizungumza baada ya kupokea jezi hiyo, Dkt. Biteko aliishukuru Yanga SC kwa kukubali mwaliko na kufika Bukombe kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi, akisema ujio wao umeleta heshima kubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo.Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa uwanja, ambao umeifanya Bukombe kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya michezo na kuendelea kufungua fursa za kiuchumi na maendeleo kwa wananchi.Mazoezi ya Yanga SC yalifanyika masaa matatu kuanzia saa 8:11 mchana hadi saa 10:11 jioni, huku yakihudhuriwa na maelfu ya mashabiki na wananchi waliokuwa wakifuatilia kwa shauku maandalizi ya timu hiyo kuelekea msimu mpya wa ligi.Mbali na mazoezi ya Yanga SC, hafla hiyo ilipambwa na burudani mbalimbali za wasanii pamoja na michezo ya utangulizi iliyohusisha timu za mpira wa miguu za wanaume na wanawake, hali iliyoongeza shamrashamra na kuifanya Bukombe Stadium kuwa kitovu cha burudani na michezo kwa siku hiyo.

Comments