KISUS AWAHIMIZA WANAMAPACHA KUENDELEZA MILA NA TAMADUNI ZA ASILI

Na,Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Wanachama wa Umoja wa Watu wa Mapacha Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamehimizwa kuendelea kuenzi mila na tamaduni za Kitanzania pamoja na kuwalea watoto katika misingi ya maadili mema ili kulinda utamaduni wa asili na kuijenga jamii yenye heshima na uwajibikaji.Wito huo umetolewa na Afisa Michezo wa Wilaya ya Bukombe, Jenipha Kisus, wakati wa hafla ya kutangaza Katiba ya Kanda ya Ziwa Magharibi ya Kikundi cha Kiutamaduni cha Watu wa Mapacha, iliyofanyika katika Kijiji cha Mtinga, Kata ya Ng'anzo, Wilaya ya Bukombe.Kisus alisema utamaduni wa watu wa mapacha ni hazina muhimu inayopaswa kuhifadhiwa kwa kuwa unafundisha watoto maadili mema, mapokezi yenye heshima, mila za asili, stadi za mapishi pamoja na kuwajengea tabia ya kuwatii wazazi na kuheshimu jamii inayowazunguka.Aidha, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kushirikiana na wazazi wa watoto mapacha na kuwapatia zawadi kama ishara ya kuthamini na kuenzi utamaduni huo pamoja na kuhamasisha malezi bora ya watoto.Alisema Dkt. Biteko ni kiongozi mwenye moyo wa kujali wananchi na anastahili kupongezwa kwa mchango wake katika kuimarisha ustawi wa jamii.

Aliongeza kuwa, mbali na kuwasaidia wazazi wa mapacha, ameendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyobadilisha sura ya Wilaya ya Bukombe, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu wa Bukombe Stadium.Kwa upande wake, Katibu wa Utamaduni wa Watu wa Mapacha Kanda ya Ziwa Magharibi, Seselo Dangamila, alisema utamaduni wa asili ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote na unapaswa kulindwa, kuenziwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.Naye Rais wa Utamaduni wa Watu wa Mapacha Kanda ya Ziwa Magharibi, Shirugu Lubigisa, alisema umoja huo umekuwa ukiadhimisha sherehe za kila mwaka tarehe 3 Agosti kwa muda wa siku nne. Alieleza kuwa mwaka huu maadhimisho hayo yamewakutanisha watu wa mapacha kutoka maeneo mbalimbali kwa lengo la kuendeleza mshikamano, kukumbushana maadili ya asili na kuhifadhi utamaduni wao kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Comments