Na, Ernest Magashi
Timu ya Katome FC imetwaa ubingwa wa Tarafa ya Bulenga katika mashindano ya KNK CUP 2026, baada ya kuichapa Ng’anzo FC kwa mikwaju ya penalti 4-2, kufuatia sare ya bila kufungana katika dakika 90 za mchezo.
Fainali hiyo iliyochezwa katika Uwanja wa Butinzya, ilizikutanisha Katome FC na Ng’anzo FC katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa, huku kila timu ikijaribu kutumia nafasi ilizopata, lakini hadi kipenga cha mwisho cha dakika 90, matokeo yalikuwa 0-0.
Kipindi cha pili kilikuwa cha kasi zaidi, huku timu zote zikiongeza mashambulizi na kutafuta bao la ushindi. Hata hivyo, safu za ulinzi za pande zote mbili zilifanya kazi kubwa ya kuwazuia washambuliaji, hali iliyosababisha mwamuzi wa mchezo, James James, kuamuru zipigwe penalti ili kumpata mshindi wa fainali hiyo.
Katika mikwaju hiyo ya penalti, Katome FC ilitumia vyema nafasi zake na kufanikiwa kushinda kwa mabao 4-2 dhidi ya Ng’anzo FC, na hivyo kutawazwa kuwa mabingwa wa Tarafa ya Bulenga katika Mashindano ya KNK CUP 2026.
Akizungumza baada ya mchezo, nahodha wa Katome FC, Pasko Wawa, alimshukuru Mungu pamoja na wachezaji wenzake kwa kujituma na kupambana hadi kufanikiwa kutwaa ubingwa huo.
Pasko alisema timu hiyo itaendelea kujituma katika hatua zinazofuata ili kutimiza azma yao ya kutwaa ubingwa wa KNK CUP 2026 katika ngazi ya Wilaya ya Bukombe.
Kwa upande wake, nahodha wa Ng’anzo FC, Sila Sila, alisema timu yake ilifanya makosa ambayo yaliwapa wapinzani nafasi ya kuibuka na ushindi, akieleza kuwa matokeo hayo yanaumiza kwa sababu hayakuwa matarajio yao.
Katika hafla ya kukabidhi zawadi, mshindi wa kwanza, Katome FC, ilikabidhiwa Shilingi 300,000 na mpira mmoja, huku mshindi wa pili, Ng’anzo FC, ikiambulia Shilingi 100,000 na mpira mmoja.
Aidha, wadau na mashabiki wa soka wa Butinzya wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kudhamini mashindano ya KNK CUP 2026, wakisema mashindano hayo yamekuwa burudani kwa wananchi na chachu ya maendeleo ya michezo kwa kuibua vipaji vya vijana na kuwaunganisha wananchi.

Comments
Post a Comment