Na, Ernest Magashi
Katome FC imeweka rekodi ya kutinga fainali ya Mashindano ya KNK CUP 2026 ngazi ya Tarafa ya Bulega baada ya kuichapa Bulega FC bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Katome.
Katome FC ilipata bao hilo dakika ya 35 kupitia mshambuliaji wake Chirwa Chirwa, aliyefumua shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Bulega FC, Ngereja Mihayo, na kuifanya Katome FC kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Katika kipindi cha pili, Bulega FC iliongeza kasi ya mashambulizi ikisaka bao la kusawazisha, lakini safu ya ulinzi ya Katome FC ilionyesha umakini mkubwa na kuendelea kulinda lango lake kwa nidhamu hadi dakika 90 zilipokamilika.
Ushindi huo umeipa Katome FC tiketi ya kucheza fainali ya KNK CUP 2026 Tarafa ya Bulega, ambapo itakutana na Ng’anzo FC katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi, Agosti 15, 2026.
Ng’anzo FC imefuzu hatua hiyo baada ya kuwaondoa mabingwa watetezi wa wilaya, Butinzya FC, kwa mikwaju ya penalti 8-7 katika mchezo mkali wa nusu fainali uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Bulega.
Fainali hiyo sasa imegeuka kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa soka katika Tarafa ya Bulega, huku Katome FC na Ng’anzo FC zikiwa na lengo moja kutwaa ubingwa wa tarafa na kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya Wilaya.
Kwa upande wa mashabiki, mchezo huo unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa kutokana na ubora ulioonyeshwa na timu zote mbili katika hatua za awali za mashindano.
KNK CUP 2026 imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza na kuibua vipaji vya michezo kutoka katika kata na maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bukombe, huku mashindano hayo yakizidi kuongeza hamasa ya michezo na kuwakutanisha wananchi kupitia michezo.

Comments
Post a Comment