Geita Gold FC imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba Jiji FC katika mchezo wa kirafiki uliochezwa usiku katika Uwanja wa Bukombe Stadium, uliopo eneo la Kilimahewa, mjini Ushirombo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Bao pekee la mchezo lilifungwa kipindi cha kwanza, na kuiwezesha Geita Gold FC kuondoka na ushindi mbele ya mamia ya mashabiki na wananchi waliojitokeza kushuhudia mchezo huo siku ya shamra shamra ya joto la kuelekea ligi kuu Tanzania Bara 2026/27.
Kipindi cha pili, Pamba Jiji FC iliongeza kasi ya mashambulizi ikisaka bao la kusawazisha, lakini ilishindwa kuipenya safu imara ya ulinzi ya Geita Gold FC hadi mwamuzi alipomaliza mchezo majira ya saa 4:00 usiku.
Kabla ya mchezo huo, Lufunga Academy ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka African Sports Youth Park. Mabao yote mawili yalifungwa kipindi cha kwanza na Frank Kavula pamoja na Aly Samson.
Katika mchezo mwingine, timu ya Watumishi wa Umma Bukombe iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Watumishi wa Umma Mbogwe. Mabao yote mawili yalifungwa kipindi cha kwanza na kiungo mshambuliaji Antony Mwalyoyo.
Kwa upande wa wanawake, timu ya Geita iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bukombe kupitia mkwaju wa penalti uliotolewa kufuatia mchezaji wa Bukombe kufanya madhambi ndani ya eneo la hatari.
Michezo hiyo ilikuwa sehemu ya shamrashamra zilizofanyika baada ya klabu ya Yanga SC kuwasili Bukombe mchana wa siku hiyo, kufanya utambulisho wa wachezaji wake na mazoezi rasmi katika Uwanja wa Bukombe Stadium kuelekea msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2026/27.Mashabiki na wadau wa soka walimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya michezo, hususan ujenzi wa Bukombe Stadium ambao umewezesha wananchi wa wilaya hiyo wanatarajia kushuhudia matukio makubwa ya michezo.
Mkazi wa Ushirombo, Lukas Paschal, alisema hakuwahi kufikiria kuwa siku moja angewaona wachezaji wa Yanga SC wakifanya mazoezi katika ardhi ya Bukombe.
"Nimefurahi sana kuona kikosi cha Yanga SC kikifanya mazoezi hapa Bukombe. Pia nampongeza Rais wa Yanga SC, Eng. Hersi Ally Said, kwa kuonesha upendo kwa kumkabidhi Mbunge wetu, Dkt. Doto Biteko, jezi rasmi ya Yanga SC ya msimu wa 2026/27. Hii ni heshima kubwa kwa Bukombe na inaonyesha namna michezo inavyozidi kukuza maendeleo ya wilaya yetu," alisema Lukas.

Comments
Post a Comment