Na, Ernest Magashi
Naibu Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, amesema mashindano ya Ngalawa Race yamekuwa miongoni mwa matukio makubwa ya michezo na burudani yaliyoipaisha na kuipamba Kizimkazi Festival 2026.
Mashindano hayo yamefanyika katika eneo la Kizimkazi, Kusini mwa Unguja, Agosti, 2026, yakishuhudiwa na ushindani mkubwa. Katika mashindano hayo, Nassor Pandu wa Mkunguni aliibuka mshindi, ikiwa ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazoendelea katika Tamasha la Kizimkazi.
“Ni dhahiri kwamba mashindano haya yamekuwa muhimu kwa vijana na jamii kwa ujumla. Tukio hili limewaleta pamoja wadau mbalimbali na kuchangia kwa kiasi kikubwa juhudi za kuboresha mazingira ya michezo na burudani,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa mashindano ya Ngalawa Race katika Kizimkazi Festival yameendelea kutoa fursa mbalimbali kwa vijana, hususan katika michezo, burudani na shughuli za kiuchumi zinazohusiana na tamasha hilo.
Kwa mujibu wa Dkt. Biteko, ushindani huo ulihusisha timu zilizofanya vizuri na kufanikiwa kufika hatua ya mwisho, ambapo timu za Mchangamle na Mkunguni ziliibuka kuwa timu mbili bora.
Amesema kila timu ilikuwa na manahodha 10, jambo linaloonyesha namna mashindano hayo yalivyoshirikisha vijana wengi na kutoa nafasi kwao kuonyesha vipaji, uwezo na ujuzi wao katika mchezo huo wa jadi wa majini.
Dkt. Biteko amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuendeleza michezo na tamaduni za asili kwa kuwa, pamoja na kutoa burudani, zinaweza kuwa chanzo cha ajira, kipato na fursa za kiuchumi kwa vijana na jamii kwa ujumla.

Comments
Post a Comment