Na, Ernest Magashi
Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, amezindua jengo jipya la Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Bukombe mkoani Geita na kuwataka watumishi wa shirika hilo, kwa kushirikiana na wananchi, kulitunza jengo pamoja na miundombinu yake ili liendelee kutoa huduma bora kwa muda mrefu.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Agosti 3, 2026, Dkt. Biteko alisema ujenzi wa jengo hilo ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa TANESCO na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi wa Bukombe na maeneo ya jirani.
Alisisitiza kuwa pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya huduma za umma, ni wajibu wa kila mtumishi na mwananchi kuhakikisha mali hizo zinatunzwa ili zidumu na kuendelea kuwanufaisha wananchi.
Dkt. Biteko alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za maendeleo zinazowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi. Alisema ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha utoaji wa huduma bora za umma.
"Tutunze jengo letu jipya la TANESCO ili liendelee kutoa huduma bora kwa muda mrefu. Miundombinu hii imejengwa kwa gharama kubwa na Serikali kwa manufaa ya wananchi, hivyo ni wajibu wetu kuilinda na kuitunza wakati wote," alisema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, alisema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya nishati ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Alieleza kuwa hadi sasa vijiji vyote 64 vya Wilaya ya Bukombe vimefikiwa na huduma ya umeme, huku Serikali ikiendelea na mpango wa kuhakikisha vitongoji vyote 348 vinapatiwa umeme ifikapo mwaka 2030.
Naye Meneja wa TANESCO Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Valerian Myula, alisema jengo hilo limejengwa kwa fedha za ndani za Shirika la Umeme Tanzania kwa gharama ya shilingi milioni 285.Mhandisi Myula alisema watumishi wa TANESCO wamepokea maelekezo ya Mbunge na Serikali kwa uzito unaostahili na kuahidi kushirikiana na wananchi katika kutunza jengo hilo pamoja na miundombinu yake.
Aliongeza kuwa jengo hilo la kisasa litaboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, kuongeza ufanisi wa utendaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja wa TANESCO katika Wilaya ya Bukombe.

Comments
Post a Comment