DKT. BITEKO AELEZEA TANZANIA ILIVYOPIGA HATUA KUBWA KATIKA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Naibu Waziri Mkuu mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, Dkt. Doto Biteko, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelea kuwa endelevu.

Dkt. Biteko aliyasema hayo wakati akishiriki mjadala kuhusu “Uongozi wa Kimkakati wa Tanzania katika Kuharakisha Mabadiliko ya Nishati Endelevu na Jumuishi,” uliofanyika katika Mdahalo wa Nishati Safi ulioandaliwa na Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) huko Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.Alisema uwepo wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ni miongoni mwa jitihada zinazotekelezwa nchini, huku akieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kutoa msukumo mkubwa kwa ajenda hiyo katika ngazi mbalimbali za uongozi, ndani na nje ya nchi.

Dkt. Biteko alisema kuendelea kuipa kipaumbele ajenda hiyo ni muhimu kutokana na ukubwa wa madhara yanayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia, ikiwemo uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa.

Alieleza kuwa takribani hekta 470,000 za misitu hupotea kila mwaka nchini kutokana na shughuli mbalimbali, ikiwemo matumizi ya kuni na mkaa, hali inayohitaji kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.

Aidha, alisema zaidi ya watu 33,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa yanayohusishwa na uchafuzi wa hewa wakati wa kupika, jambo linaloonesha umuhimu wa kuharakisha mpito kutoka kwenye nishati isiyo safi kwenda kwenye nishati safi ya kupikia.Aliongeza kuwa matumizi ya nishati isiyo safi yana athari pia katika ustawi wa wanawake na watoto. Kwa upande wa wanawake, alisema muda mwingi hutumika kutafuta kuni badala ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wa watoto, Dkt. Biteko alisema baadhi yao hukosa muda wa kutosha wa kuhudhuria masomo kutokana na kulazimika kuwasaidia wazazi au familia zao kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia.

Katika mjadala huo, Dkt. Biteko alisisitiza umuhimu wa kufanya tathmini za mara kwa mara ili kubaini kiwango cha uendelevu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususan baada ya wananchi kuwezeshwa kupata teknolojia na miundombinu inayohitajika.

Alisema tathmini hizo zitaiwezesha Serikali na wadau kubaini changamoto zinazojitokeza, kupima matokeo yaliyofikiwa na kuweka mikakati madhubuti zaidi ya kuendeleza matumizi ya nishati safi, salama na endelevu ya kupikia nchini.

Dkt. Biteko pia aliipongeza Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) kwa kuwa miongoni mwa taasisi zinazochangia utekelezaji wa Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia shughuli mbalimbali, ikiwemo kusaidia upatikanaji wa miundombinu na kuandaa midahalo inayowakutanisha wadau kujadili namna bora ya kuharakisha matumizi ya nishati safi, salama na endelevu nchini.

Comments