Na, Ernest Magashi
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Mhadis Paskas Muragili, amewapongeza viongozi wa Taasisi ya Itumikie Nchi Yako Tanzania (INYATA) Wilaya ya Bukombe Mkoa wa Geita, kwa kuja na ajenda ya kuhamasisha amani, uzalendo na uwajibikaji katika jamii.
Pongezi hizo zilitolewa na Mhadis Muragili wakati wa kuwapokea na kufanya utambulisho wa viongozi hao wa INYATA Wilaya ya Bukombe ofisini kwake. Viongozi hao waliongozana na Mwenyekiti wa INYATA Mkoa wa Geita, John Alphonce sumuni.
Mhadis Muragili alisema serikali iko tayari kushirikiana na INYATA katika kutekeleza majukumu yake, hususan katika kuhamasisha wananchi kuilinda nchi, kudumisha amani na kujenga jamii yenye uzalendo na mshikamano.
Aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia malengo, kanuni na miongozo ya taasisi hiyo, pamoja na kufuata sheria na taratibu za nchi ili kuendelea kupata ushirikiano kutoka serikalini.
“Tunayo kazi ya kufanya kuhakikisha kwa pamoja tunaendelea kuhamasisha wananchi kulinda amani na utulivu wa nchi. Taasisi inapokuja na malengo mazuri kama haya, ni muhimu viongozi wake kubaki kwenye mwelekeo walioujiwekea na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu,” alisema Mhadis Muragili.
Aidha, Mhadis Muragili aliwataka viongozi wa INYATA kufanya kazi kwa kuzingatia malengo ya taasisi hiyo na kutotoka nje ya mipaka ya majukumu yao, akisisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu wa nchi.
Kwa upande wake, Katibu wa INYATA Wilaya ya Bukombe, Dida Kisika ikungula. alisema taasisi hiyo itaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa amani, huku ikiwahamasisha vijana kuwa mstari wa mbele katika kuitunza na kuilinda.
Naye Makamu Mwenyekiti wa INYATA Wilaya ya Bukombe, Joseph Mpozemenya, alisema wataendelea kufanya kazi kwa ukaribu na serikali na kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kulinda amani na utulivu wa nchi.
Mpozemenya alisema INYATA haitamvumilia mwanachama atakayekiuka kanuni na taratibu za taasisi hiyo, akieleza kuwa hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa taratibu, ikiwemo kufutiwa uanachama kwa atakayebainika kwenda kinyume na misingi ya taasisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa INYATA Mkoa wa Geita, John Alphonce sumuni. alisema viongozi wa taasisi hiyo wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni na miongozo ya INYATA pamoja na kuheshimu sheria na taratibu za nchi.
Alphonce sumuni alisema lengo lao ni kuhakikisha jamii inaendelea kulinda amani, kudumisha upendo, mshikamano na uzalendo, huku kila mwananchi akitambua wajibu wake katika kujenga Tanzania yenye amani na utulivu.

Comments
Post a Comment