BUKOMBE STAR YATWAA UBINGWA WA KNK CUP 2026 KATA YA BUKOMBE KWA KUICHAPA BARCELONA FC BAO 1-0


Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Bukombe Star imeibuka bingwa wa mashindano ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Bukombe, Tarafa ya Bukombe, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, baada ya kuichapa Barcelona FC kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Bukombe.

Mchezo huo wa fainali uliokuwa na ushindani mkubwa uliwakutanisha timu mbili zilizoonyesha kiwango cha juu tangu kuanza kwa mashindano. Hata hivyo, Bukombe Star ilitumia vyema nafasi zake na kufanikiwa kupata bao pekee lililoihakikishia ubingwa wa KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Bukombe.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Diwani wa Kata ya Bukombe, Rozalia Masokola, kwa niaba ya mdhamini wa mashindano hayo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, aliwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki kwa kuonyesha ushindani wa hali ya juu na kudumisha amani katika kipindi chote cha mashindano.

Alisema mashindano ya KNK Cup yameendelea kuwa chachu ya kuibua na kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa wananchi na kuendeleza sekta ya michezo katika Wilaya ya Bukombe.Katika hafla ya kukabidhi zawadi, mabingwa Bukombe Star walizawadiwa seti moja ya jezi, mpira mmoja na fedha taslimu shilingi 100,000. Nao washindi wa pili, Barcelona FC, walikabidhiwa mpira mmoja pamoja na fedha taslimu shilingi 50,000.Mashindano ya KNK Cup 2026 yanaendelea katika kata mbalimbali za Wilaya ya Bukombe yakilenga kuibua vipaji vya soka, kuhamasisha ushiriki wa vijana katika michezo na kuimarisha mshikamano wa jamii kupitia michezo.

Comments