Bugelenga FC imetwaa ubingwa wa Tarafa ya Bukombe katika mashindano ya KNK CUP 2026 baada ya kuichapa Shigulumule FC kwa mikwaju ya penalti 5-4, kufuatia timu hizo kutoshana nguvu ndani ya dakika 90 za mchezo wa fainali.
Katika mchezo huo wa fainali uliowakutanisha mabingwa wa kata Bugelenga FC ilionyesha kiwango kizuri cha soka huku Shigulumule FC nayo ikicheza kwa ushindani mkubwa, kila timu ikijaribu kutafuta bao la ushindi.
Hata hivyo, juhudi za timu hizo hazikuzaa matunda ndani ya dakika 90, hali iliyomlazimu mwamuzi wa kati kuamuru mikwaju ya penalti kwa mujibu wa kanuni za mashindano ili kumpata bingwa wa Tarafa ya Bukombe.
Katika mikwaju hiyo ya penalti, Bugelenga FC ilifanikiwa kuwa bora zaidi kwa kushinda kwa mabao 5-4 na kutawazwa kuwa mabingwa wa Tarafa ya Bukombe katika KNK CUP 2026.
Kwa ushindi huo, Bugelenga FC ilikabidhiwa zawadi ya Shilingi 300,000 pamoja na mpira mmoja, huku mshindi wa pili, Shigulumule FC, akipokea Shilingi 100,000 na mpira mmoja.
Bugelenga FC sasa inaelekeza nguvu zake katika hatua inayofuata ya mashindano, ambapo itawakilisha Tarafa ya Bukombe katika kuwania ubingwa wa Wilaya.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Katibu wa Kamati ya Mashindano ya KNK CUP 2026, Domisian Kabalenga, alimpongeza mdhamini wa mashindano hayo, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhami mashindano hayo.
Kabalenga alisema KNK CUP imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wananchi, kukuza michezo na kuibua vipaji vya vijana katika maeneo mbalimbali ya Bukombe.

Comments
Post a Comment