Wanawake mkoani Geita wametakiwa kuwatii, kuwaheshimu na kuwanyenyekea waume zao, pamoja na kuachana na tabia za kurithi mienendo ya wazazi wao ambayo inaweza kusababisha migogoro katika ndoa na kuongeza idadi ya watoto wanaolelewa mitaani.
Wito huo umetolewa na Askofu wa Kanisa la Ufunuo Jimbo la Geita, Rosemeri Mashauri, wakati wa ibada takatifu ya mafundisho ya ndoa iliyofanyika katika Kanisa la Ufunuo mjini Ushirombo.
Askofu Mashauri alisema ndoa nyingi zinavunjika kutokana na baadhi ya wanawake kutokuwa tayari kujishusha na kuheshimu waume zao, huku wakijiona kuwa na haki zaidi ndani ya nyumba na kutaka kuendesha ndoa zao kwa kufuata mifumo waliyoiona katika familia walizotoka.
Alisema baadhi ya wanawake wanapoolewa huendelea na tabia walizozikuta kwa wazazi wao, hali ambayo inaweza kuleta migogoro katika ndoa pale wanapokutana na waume wenye mitazamo tofauti.
Aliwataka wanawake kuwapenda na kuwaheshimu waume zao, huku akiwashauri kuachana na tabia za kurithi kutoka kwa wazazi wao na badala yake kujenga ndoa kwa kufuata misingi ya upendo, heshima, uvumilivu na maelewano.
“Umeolewa, unatoka na tabia za kwenu. Mwanamume anataka uishi hivi, wewe unataka uishi kama kwenu. Kama wazazi wanapigana au baba anashurutishwa na wewe unataka kushurutisha, hakika wanaume wengine hawapendi,” alisema Askofu Mashauri.
Aidha, Askofu Mashauri aliwataka wanaume kutokata tamaa mapema katika ndoa, bali waendelee kuzilea familia zao kwa kuzingatia maadili ya kifamilia, kuwalea na kuwasomesha watoto.
Aliwashauri wanaume wanapokutana na changamoto katika ndoa kutowatelekeza wake na watoto, bali kuwashirikisha wazazi pamoja na viongozi wa dini ili kutafuta suluhisho la migogoro na kuepusha ongezeko la watoto wanaolelewa mitaani.
Askofu Mashauri alisema wanawake wanapaswa kuelewa kuwa ndoa inahitaji mwenza mwenye tabia njema, anayeheshimu na kumtii mwenzake, akisisitiza kuwa ndoa haipaswi kujengwa kwa kuangalia sura pekee.
Alitoa mfano wa baadhi ya tabia ambazo mtu anaweza kuziona katika familia alikokulia na kuamua kuzihamishia katika ndoa yake bila kuzingatia mazingira ya familia mpya.
“Kwa mfano, binti akiwa nyumbani anaona baba anasafisha nyumba, anaosha vyombo au anafanya kazi nyingine za nyumbani, anapoolewa anaweza kutaka mume wake afanye vivyo hivyo. Lakini kama mume huyo hakulelewa katika mazingira hayo, inaweza kusababisha kutokuelewana na kuumiza hisia za wanandoa,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kinamama wa Kanisa la Ufunuo Ushirombo, Pirisca Chando, alimpongeza Askofu Mashauri kwa mafundisho hayo na kuwataka wanawake kuwa wanyenyekevu na kuzingatia mafundisho yaliyo katika Maandiko Matakatifu ili kujenga familia na jamii yenye maadili mema.
Naye muumini wa Kanisa la Ufunuo Ushirombo, Daniel Hereniko, alishukuru uongozi wa Jimbo la Geita kwa kutoa mafundisho hayo, akisema yamegusa changamoto zinazowakabili wanawake na wanaume katika maisha ya ndoa, ikiwemo changamoto za kiuchumi.
Alisema mafundisho hayo ni muhimu kwa wanandoa kwani yanaweza kusaidia kujenga familia zenye upendo, heshima, mshikamano na malezi bora ya watoto.

Comments
Post a Comment