Askofu wa Kanisa la Ufunuo Jimbo la Geita, Rosemeri Mashauri, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa ushirikiano wake na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo uliofanikisha ujenzi wa Bukombe Stadium, akisema mradi huo utakuza michezo, kuibua vipaji vya vijana na kuchochea uchumi wa wananchi.
Askofu Mashauri alitoa pongezi hizo wakati wa ibada maalumu iliyolenga kuwafundisha wazazi na walezi kuhusu wajibu wao wa kulea watoto katika maadili mema na kuwahimiza vijana kuwathamini wazazi wao badala ya kuwatelekeza vijijini wakikimbilia mijini bila kuwajibika.
Alisema pamoja na miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa Bukombe, uongozi wa Dkt. Biteko umeendelea kuleta mabadiliko makubwa yanayoonekana wazi, huku Bukombe Stadium ikitarajiwa kuongeza thamani ya mji wa Ushirombo na kufungua fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara na wajasiriamali.
Naye Askofu wa Kanisa la Ufunuo kutoka Ofisi ya Askofu Mkuu Tanzania, Elizabeth Mkumbo, alimpongeza Askofu Rosemeri Mashauri na waumini wa Jimbo la Geita kwa kuendelea kushirikiana na viongozi wa Serikali na kuthamini juhudi zinazofanyika katika kuleta maendeleo ya wananchi.
Pia aliwahimiza waumini kuendelea kudumisha upendo, umoja na mafundisho ya Neno la Mungu, huku akisisitiza umuhimu wa kuwaheshimu na kuwatunza wazazi ili kuendelea kupokea baraka za Mungu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Kanisa la Ufunuo Tanzania, Jeremia Fimbo, alisema viongozi wa Kanisa wamefurahishwa na mapokezi mazuri waliyopata Jimbo la Geita pamoja na kuona maendeleo makubwa yanayotekelezwa kupitia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Mbunge wa Bukombe, Dkt. Doto Biteko.
Alisema Bukombe imepiga hatua kubwa za maendeleo, ikiwemo ujenzi wa Bukombe Stadium, ambao unatarajiwa kuwa kitovu cha michezo na shughuli mbalimbali za kijamii.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadis Paskas Muragili, ametangaza rasmi viingilio vya shamra shamra za kuelekea msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2026/27 zitakazofanyika Agosti 4, 2026 katika Bukombe Stadium.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 31, 2026, Muragili alisema viingilio vitakuwa kama ifuatavyo:Mzunguko: Shilingi 10,000Jukwaa la Ushirombo na Jukwaa la Siloka: Shilingi 20,000 VIP A: Shilingi 50,000 VIP B: Shilingi 100,000 VVIP: Shilingi 150,000.
Alisema tiketi zinapatikana kupitia mfumo wa mtandao na vituo mbalimbali ikiwemo The One na Kitamba OG mjini Ushirombo, huku nje ya mji zikipatikana katika Mgodi wa Msasa, Katoro, Masumbwe na Geita Mjini.Pia, kuna mpango wa kuongeza vituo vya mauzo Kahama, Chato na Mwanza kutokana na idadi kubwa ya mashabiki wanaotarajiwa kuhudhuria.
Muragili aliwahimiza wananchi wa Bukombe na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo, akieleza kuwa burudani zitaanza saa 2:30 asubuhi na kuendelea hadi saa 3:00 usiku.
Aidha, mageti nane yatakuwa wazi ili kurahisisha mashabiki kuingia uwanjani.Aliongeza kuwa Bukombe Stadium imejengwa kwa viwango vya kisasa na ina uwezo wa kuchukua mashabiki zaidi ya 5,000, wakiwemo zaidi ya 4,000 watakaokaa kwenye viti na zaidi ya 1,000 watakaotazama wakiwa wamesimama.

Comments
Post a Comment