WAJASIRIAMALI WAMTAJA DKT. BITEKO KUCHOCHEA UCHUMI WAO KUPITIA MASHINDANO YA KNK CUP

Na,Ernest Magashi 

ebukombesasablogspot.com.tz

Wajasiriamali mbalimbali wilayani Bukombe, mkoani Geita, wamesema mashindano ya KNK Cup yanayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Mashaka Biteko, yamekuwa chachu ya kukuza biashara zao na kuongeza kipato kutokana na ongezeko la mashabiki wanaohudhuria viwanjani.Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wajasiriamali hao walisema mashindano hayo yameongeza mzunguko wa fedha katika maeneo yanayochezewa mechi, hali iliyowawezesha kuuza bidhaa nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya kuanza kwa mashindano.Mjasiriamali wa vinywaji katika Kata ya Ushirombo, Monica Samwel, alisema siku za mechi huuza bidhaa zake zote na kwa sasa hupata mauzo ya wastani wa Shilingi 50,000 kwa siku, tofauti na awali ambapo alikuwa akipata takribani Shilingi 26,000.Kwa upande wake, Siyawezi Pius alisema kupitia KNK Cup mauzo yake yameongezeka na sasa hupata hadi Shilingi 80,000 kwa siku, ilhali kabla ya mashindano alikuwa akiishia kupata takribani Shilingi 38,000.Naye mjasiriamali wa matunda, hususan miwa, katika Uwanja wa Katente, Sadock Bonje, alisema faida aliyopata kupitia biashara wakati wa mashindano imemwezesha kuwanunulia watoto wake mahitaji ya shule ikiwemo viatu, jambo alilosema ni ushahidi kuwa michezo inaweza kuwa fursa ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.Katika Kata ya Busonzo, mjasiriamali Sikitu Thomas alisema biashara yake ya mahindi ya kuchemsha imeongezeka kwa kiwango kikubwa, ambapo kwa sasa huuza ndoo mbili kwa siku na kupata faida ya takribani Shilingi 47,000, tofauti na awali alipokuwa akipata kati ya Shilingi 14,000 na 16,000 kwa siku.Akizungumzia mafanikio ya mashindano hayo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Busonzo pia msimamizi mkuu wa mashindano, Remember Mfaume, alisema KNK Cup imekuwa zaidi ya mashindano ya mpira wa miguu kwani imeunganisha wananchi, imeibua vipaji vya vijana na wakati huohuo imeongeza kipato cha wajasiriamali wanaofanya biashara viwanjani.Alisema mafanikio hayo yanaonyesha kuwa uwekezaji katika michezo unaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika jamii, huku akimpongeza Dkt. Doto Biteko kwa kuanzisha mashindano hayo ambayo yameleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Bukombe.

Comments