Wajasiriamali wadogo wa Ushirombo, wilayani Bukombe mkoani Geita, wameeleza jinsi mashindano ya KNK CUP 2026, yanayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, yalivyowaongezea kipato na kuchochea ukuaji wa biashara zao.
Akizungumza katika Uwanja wa Michezo wa Kata ya Katente, mfanyabiashara wa matunda, Jackson Peter, alisema mashindano hayo yamekuwa chachu ya kuinua uchumi wa wajasiriamali wanaofanya biashara viwanjani wakati wa michezo.
Alisema kabla ya kuanza kwa mashindano alikuwa akiuza matunda yenye thamani ya wastani wa shilingi 4,000 kwa siku, lakini kwa sasa mauzo yake yameongezeka na kufikia wastani wa shilingi 35,000 kwa siku.
"Nimekuwa nikifanya biashara kwenye viwanja vya michezo ya ligi ya KNK CUP kila mwaka, na mashindano haya yameniongezea wateja pamoja na kipato. Yamenisaidia kukuza biashara yangu kwa kiwango kikubwa," alisema Peter.
Kwa upane wake, mfanyabiashara wa nguo Philipo Thomas alisema amekuwa akipata faida kubwa kwa kuuza nguo wakati wa michezo, jambo ambalo limemwezesha kuongeza mapato yake.
Alieleza kuwa kabla ya mashindano hayo alikuwa akipata wastani wa shilingi 5,700 kwa siku, lakini kwa sasa hupata mauzo yanayozidi shilingi 100,000 kwa siku kutokana na idadi kubwa ya mashabiki wanaohudhuria viwanjani.Thomas alimpongeza Dkt. Doto Biteko kwa kuendelea kuandaa na kudhamini mashindano hayo, akisema yamefungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wajasiriamali wa eneo hilo.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Katente, David Jeremia, alisema KNK CUP imekuwa zaidi ya mashindano ya michezo, kwani imekuwa jukwaa la kuwakutanisha wananchi, kuwapa burudani bila kiingilio na wakati huohuo kuwawezesha wafanyabiashara kuongeza kipato cha familia zao.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Katente, Kasuluzu Ng'hwani, alisema lengo la Mbunge Dkt. Doto Biteko ni kutumia michezo kama nyenzo ya kuimarisha mshikamano wa wananchi, kuibua vipaji vya vijana na kuhamasisha shughuli za kiuchumi kupitia biashara zinazofanyika wakati wa mashindano.
Mashindano ya KNK CUP 2026 yameendelea kuvutia maelfu ya mashabiki kutoka kata mbalimbali za Wilaya ya Bukombe, huku yakitoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo kuongeza mauzo, ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa wananchi.

Comments
Post a Comment