ebukombesasablogspot.com.tz
Wadau wa michezo wa Kata ya Busonzo, Tarafa ya Siloka, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameongeza hamasa katika fainali ya mashindano ya KNK Cup 2026 kwa kutoa zawadi mbalimbali kwa timu zilizoshika nafasi ya kwanza hadi ya nne, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za mdhamini wa mashindano hayo, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.
Kwa niaba ya Meneja wa TFS Wilaya ya Bukombe, Afisa Misitu wa TFS, Bakari Mboga, alikabidhi jumla ya shilingi 100,000, ambapo Mabatini FC iliyomaliza katika nafasi ya tatu ilipokea shilingi 50,000, huku Engodhehama FC iliyoshika nafasi ya nne ikikabidhiwa shilingi 50,000. Jumla ya timu 16 zilishiriki mashindano hayo ya kusaka ubingwa wa Kata ya Busonzo.
Mboga alimpongeza Dkt. Biteko kwa kuanzisha KNK Cup, akisema mashindano hayo yamekuwa chachu ya kuimarisha umoja na mshikamano wa wananchi pamoja na kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana kupitia michezo.
Naye mdau wa michezo, Dickson Kivuyo, aliongeza zawadi kwa bingwa wa Kata ya Busonzo, Nampalahala FC, kwa kuikabidhi mpira mmoja, huku mshindi wa pili, Idoselo Warriors, akikabidhiwa pea moja ya viatu
Kivuyo alisema ameridhishwa na namna Dkt. Biteko alivyoandaa mashindano hayo, hivyo akaamua kutoa zawadi hizo kama ishara ya kuwatia moyo wachezaji wa timu zote mbili zilizofika hatua ya fainali.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Busonzo ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mashindano ngazi ya kata, Rehema Mfaume, aliwapongeza wadau wa michezo kwa kuunga mkono KNK Cup kwa kuongeza zawadi kwa timu zilizofanya vizuri.
Alisema hatua hiyo imeongeza thamani ya mashindano, imewapa motisha wachezaji na kuleta furaha kwa viongozi pamoja na wananchi wa Kata ya Busonzo.
Akikabidhi zawadi za mdhamini kwa niaba ya Diwani wa Kata ya Busonzo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nalusungute, Kasema Mashauri, alimpongeza Dkt. Doto Biteko kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya michezo kupitia KNK Cup, akisema mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kutambua na kukuza vipaji vya vijana.
Katika zawadi za mdhamini, bingwa Nampalahala FC alikabidhiwa seti moja ya jezi, mpira mmoja na shilingi 100,000, huku mshindi wa pili, Idoselo Warriors, akijinyakulia mpira mmoja na shilingi 50,000, sambamba na bonasi zilizotolewa na wadau wa michezo.
Katika mchezo wa fainali uliochezwa Julai 20, 2026 kwenye Uwanja wa Michezo Busonzo, Nampalahala FC ilitwaa ubingwa wa KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Busonzo baada ya kuichapa Idoselo Warriors kwa bao 1-0.
Nahodha wa Nampalahala FC, Mateso Kabadi, alimshukuru Dkt. Doto Biteko kwa kuandaa mashindano hayo na kutoa zawadi zenye motisha, huku pia akiwapongeza wadau wa michezo walioongeza zawadi, akisema zimeongeza ari na hamasa kwa wachezaji.
Kwa upande wake, nahodha wa Idoselo Warriors, Mwanyas Edwin, alimshukuru Dkt. Biteko pamoja na wadau wa michezo kwa zawadi walizotoa, akieleza kuwa zimeonyesha kuthamini juhudi za wachezaji bila kujali matokeo ya uwanjani
Viongozi wa Mabatini FC na Engodhehama FC, zilizomaliza katika nafasi ya tatu na ya nne, walieleza kufurahishwa na zawadi walizopokea kutoka kwa wadau wa michezo, wakisema hawakutarajia kuthaminiwa licha ya kutolewa kabla ya kufika fainali. Walisema hatua hiyo itawaongezea morali ya kujiandaa vizuri zaidi kwa mashindano yajayo.

Comments
Post a Comment