Na, Ernest Magashi
Wadau wa michezo wa Kata ya Bulangwa, Tarafa ya Ushirombo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya KNK Cup, wakisema yamekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa wananchi na kutoa burudani kwa jamii.
Pongezi hizo zilitolewa wakati wa fainali ya KNK Cup ngazi ya Kata ya Bulangwa iliyozikutanisha Ushirombo Warriors na Ashanti FC katika Uwanja wa Bulangwa. Baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 1-1 ndani ya dakika 90 za mchezo, bingwa alipatikana kwa mikwaju ya penalti ambapo Ushirombo Warriors iliibuka na ushindi wa penalti 5-4 na kutwaa ubingwa wa kata.
Mmoja wa wadau wa michezo, Thomas James, alisema Dkt. Biteko ameendelea kuonyesha dhamira ya kuendeleza michezo kwa kuandaa mashindano yanayowakutanisha wananchi na kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.
Naye Patrick Jackson alisema KNK Cup imekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya michezo wilayani Bukombe, akibainisha kuwa Dkt. Biteko amekuwa akitenga muda wa kufuatilia michezo hiyo jambo linalowapa hamasa wachezaji na wadau wa soka.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Bulangwa na msimamizi mkuu wa mashindano hayo ngazi ya kata, Eunice Odinga, alimkabidhi nahodha wa Ushirombo Warriors zawadi ya ubingwa iliyojumuisha seti moja ya jezi na shilingi 100,000, huku Ashanti FC ikipewa mpira mmoja na shilingi 50,000 kwa kumaliza katika nafasi ya pili.
Odinga alimshukuru Mungu kwa mashindano hayo kumalizika salama, akieleza kuwa timu 10 zilishiriki kuanzia Julai 1 hadi Julai 17, 2026.
"Nimpongeze Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano haya kila mwaka. Yamekuwa yakibua vipaji na kuwapa vijana fursa ya kuonyesha uwezo wao kupitia michezo," alisema Odinga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya KNK Cup 2026, Nelyvin Ndugu, alisema kukamilika kwa fainali za kata ni hatua muhimu kuelekea hatua zinazofuata za mashindano ngazi ya Tarafa na wilaya.
Aliwahamasisha wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kushuhudia michezo iliyobaki, akisema ushiriki wao unaonyesha kuunga mkono juhudi za mdhamini wa mashindano, Dkt. Doto Biteko.
Mashindano ya KNK Cup 2026 yalianza Julai 1, 2026 katika kata zote za Wilaya ya Bukombe, yakishirikisha jumla ya timu 248 zilizosajiliwa, huku hatua za mashindano zikiendelea katika ngazi mbalimbali hadi kupatikana bingwa wa wilaya.

Comments
Post a Comment