Timu ya Ushirombo Warriors imeendelea kuthibitisha ubora wake katika mashindano ya KNK Cup 2026 baada ya kuichapa Ushirombo Star mabao 3-0 na kufuzu hatua ya nusu fainali ya kata.
Mchezo huo wa robo fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Kata ya Bulangwa ulikuwa na ushindani mkubwa, huku ukizikutanisha timu hizo mbele ya mamia ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia pambano hilo. Licha ya mchezo kuwa wa kuvutia, ulitawaliwa pia na matukio ya kinidhamu baada ya mchezaji wa Ushirombo Warriors, Magazi Doto, na mchezaji wa Ushirombo Star, Maduhu Maduhu, kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia kurushiana ngumi.
Ushirombo Warriors walipata bao la kwanza kupitia kwa Juma Julius dakika ya 46, kabla ya Siras Lupogo kuongeza la pili dakika ya 56. Gabriel Bigilimana alihitimisha ushindi huo kwa kufunga bao la tatu dakika ya 74.
Kwa ushindi huo, Ushirombo Warriors imekata tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali ya kata, huku Ushirombo Star ikiaga rasmi mashindano ya KNK Cup 2026.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Bulangwa na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, Peter Mkina, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya KNK Cup ambayo yamekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana na kukuza mchezo wa soka wilayani humo.
Mkina alisema mashindano hayo yameendelea kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Wilaya ya Bukombe, huku yakitoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao, kujitangaza na kuwavutia wadau mbalimbali wa michezo. Aidha, aliwataka wachezaji kuendelea kuzingatia nidhamu na kucheza kwa kufuata sheria za mchezo ili kulinda heshima ya mashindano hayo.

Comments
Post a Comment