USHIROMBO WARRIORS YAICHAPA BULANGWA FC 2-1, YATINGA FAINALI YA KATA KNK CUP 2026


Na, Ernest Magashi 

ebukombesasablogspot.com.tz

Ushirombo Warriors imefanikiwa kutinga fainali ya Kata ya Bulangwa katika mashindano ya KNK Cup 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Bulangwa FC katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Kata ya Bulangwa.Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulivuta mamia ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia timu hizo zikisaka tiketi ya kucheza fainali.Ushirombo Warriors ilianza vyema mchezo huo baada ya Bomba Bomba kuifungia timu yake bao la kuongoza katika dakika ya 17. Hata hivyo, Bulangwa FC ilisawazisha kupitia kwa Zachalia Frasenc aliyetikisa nyavu katika dakika ya 34 na kufanya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare ya bao 1-1.Kipindi cha pili kilikuwa na presha kubwa kutoka kwa timu zote, lakini Ushirombo Warriors ilifanikiwa kupata bao la ushindi katika dakika ya 84 kupitia kwa Samata Samwel, aliyehitimisha shambulizi zuri na kuihakikishia timu yake ushindi wa mabao 2-1 pamoja na tiketi ya kutinga fainali ya kata.Kwa ushindi huo, Ushirombo Warriors imeendelea kuonyesha ubora wake katika mashindano hayo, huku Bulangwa FC ikihitimisha safari yake ya KNK Cup 2026 licha ya kupambana kwa nguvu katika dakika zote 90 za mchezo.Akizungumza baada ya mchezo huo, Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Bulangwa na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, Peter Mkina, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya KNK Cup ambayo amesema yamekuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya vijana na kukuza mchezo wa soka wilayani Bukombe.Mkina alisema mashindano hayo yameendelea kuimarisha umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wananchi, huku yakitoa fursa kwa wachezaji kujitangaza na kuvutia wadau mbalimbali wa michezo. Aidha, aliwataka wachezaji kuendelea kuzingatia nidhamu, kucheza kwa kufuata sheria za mchezo na kulinda hadhi ya mashindano hayo.

Comments