USHIROMBO WARRIORS NA ASHANTI FC KUPIGANIA TIKETI YA TARAFA KATIKA FAINALI YA KATA YA BULANGWA KNK CUP 2026


Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Macho na masikio ya mashabiki wa soka kata ya Bulangwa wilayani Bukombe mkoani Geita, sasa yanaelekezwa katika Uwanja wa Michezo wa Kata ya Bulangwa, ambapo Ushirombo Warriors na Ashanti FC zitashuka dimbani Julai 17, 2026 kupambana katika fainali ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Bulangwa.Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa, huku timu zote zikisaka ushindi utakaowapa tiketi ya kuwakilisha Kata ya Bulangwa katika hatua ya Tarafa ya Ushirombo.Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Bulangwa na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, Peter Mkina, amesema fainali hiyo itawakutanisha timu mbili zenye ubora na ushindani mkubwa, hali inayotarajiwa kuvutia mamia ya mashabiki kujitokeza kushuhudia pambano hilo.Mkina pia alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya KNK Cup, akisema yamekuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya vijana, kukuza soka la wilaya na kuimarisha mshikamano wa wananchi.Ushirombo Warriors ilikata tiketi ya fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Bulangwa FC katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Julai 13, 2026.Kwa upande wa Ashanti FC, ilitinga hatua hiyo baada ya kuiondosha Lufuna FC kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 4-1, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 za mchezo wa nusu fainali uliochezwa Julai 14, 2026.Kwa mujibu wa Mkina, timu zote mbili zina vikosi imara na mashabiki wengi, jambo linaloashiria kuwa fainali hiyo itakuwa ya kuvutia na yenye ushindani wa hali ya juu. Timu itakayoshinda itafuzu kuendelea na mashindano ya KNK Cup 2026 ngazi ya Tarafa ya Ushirombo.Aidha, amewataka wachezaji kucheza kwa nidhamu, kuheshimu sheria za mchezo na kulinda hadhi ya mashindano hayo, akisisitiza kuwa KNK Cup imeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya michezo, kuibua vipaji na kutoa fursa kwa wachezaji kujitangaza mbele ya wadau mbalimbali wa soka.

Comments