Timu ya salama FC imeendelea kuonyesha kiwango bora katika mashindano ya KNK Cup 2026 baada ya kuichapa Mwenge FC mabao 2-0 na kufuzu hatua inayofuata ya mashindano hayo yanayoendelea katika kata zote 17 za Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.
Katika mchezo huo wa sita, Usalama FC ilianza kuonyesha makali yake mapema ambapo Jacob Maisha aliifungia timu yake bao la kwanza dakika ya 16. Bao la pili lilifungwa na Emmanuel Kimisha dakika ya 70, na kuifanya Usalama FC kuondoka na ushindi muhimu.
Licha ya Mwenge FC kuongeza kasi na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara katika kipindi cha pili wakisaka mabao ya kurejea mchezoni, safu ya ulinzi ya Usalama FC ilisimama imara na kudhibiti hatari zote hadi mwamuzi alipopuliza kipyenga cha mwisho.
Ushindi huo umeifanya Usalama FC kusonga mbele katika hatua inayofuata ya KNK Cup 2026, huku Mwenge FC ikiaga rasmi mashindano hayo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Vijana wa UVCCM Kata ya Katente na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, Devid Jeremia, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya KNK Cup ambayo amesema yamekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa jamii na kutoa burudani kwa wananchi.
Jeremia alisema kuwa katika Kata ya Katente zilisajiliwa timu 12, ambapo baada ya michezo ya hatua ya awali timu sita zimefanikiwa kufuzu moja kwa moja hatua inayofuata, huku timu nyingine zikisubiri nafasi ya kuendelea kupitia mfumo wa Best Losers.
Aidha, aliwahamasisha wananchi na mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Michezo wa Katente kushuhudia michezo iliyosalia ya KNK Cup 2026. Pia alizitaka timu zote zinazoshiriki kuzingatia muda, sheria na kanuni za mashindano ili kudumisha nidhamu, ushindani wa haki na kuendeleza maendeleo ya michezo wilayani Bukombe.
Naye Diwani wa Kata ya Katente, Kasuluzu Ng'hwani, aliwataka vijana kuendelea kutumia mashindano hayo kama fursa ya kuonyesha vipaji vyao na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha maendeleo yao. Alimshukuru Dkt. Doto Biteko kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya michezo kupitia KNK Cup 2026, akisema mashindano hayo yameleta hamasa kubwa kwa vijana na wananchi wa Bukombe.

Comments
Post a Comment