Na,Ernest Magashi
Mashindano ya KNK Cup 2026 yameingia katika hatua ya mwisho ngazi ya kata baada ya timu 16 kufuzu kucheza fainali za kata, huku timu 232 zikiaga rasmi mashindano hayo.
Akizungumza na Bukombe Sasa Media, Katibu wa Kamati ya Mashindano ya KNK Cup 2026, Domisian Kabalenga, alisema kati ya timu 248 zilizoanza mashindano hayo, ni timu 16 pekee zilizofanikiwa kutinga fainali za kata, ambazo zitaanza kuchezwa kuanzia Julai 16, 2026.
Alisema kila bingwa wa kata atajinyakulia zawadi na kupata tiketi ya kuiwakilisha kata yake katika hatua ya Tarafa, ambapo kutakuwa na tarafa nne zitakazoshindanishwa kwa mfumo wa mtoano hadi kupatikana mabingwa wa kila tarafa.
"Kutoka hapo tutapata timu nne bora zitakazocheza hatua ya mwisho kuwania ubingwa wa Jimbo la Bukombe katika mashindano ya KNK Cup 2026," alisema Kabalenga.
Aliwataka viongozi wa timu kuhakikisha vikosi vyao vinafika uwanjani kwa wakati, huku akiwasisitiza waamuzi kusimamia sheria za mchezo kwa haki na weledi ili mashindano yaendelee katika mazingira ya amani, upendo na ushindani wa haki.
"Michezo ni afya, urafiki na umoja. Tunatarajia kuona fainali zenye ushindani mkubwa lakini zenye nidhamu na kuheshimiana," aliongeza.
Mashindano ya KNK Cup 2026 yanadhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, ambaye ameendelea kupongezwa kwa mchango wake katika kuinua sekta ya michezo wilayani humo.
Wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo uliofanyika Julai 1, 2026 katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Runzewe, Kata ya Uyovu, madiwani mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe walieleza kuwa KNK Cup imekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha afya za wananchi na kukuza mshikamano katika jamii.
Diwani wa Kata ya Uyovu, Mathayo Kagoma, alisema mashindano hayo, ambayo hapo awali yalijulikana kama Doto Cup, yamezalisha wachezaji wengi wenye vipaji na kufungua fursa za ajira kupitia michezo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema baadhi ya vijana waliopitia KNK Cup tayari wanacheza katika timu zinazoshiriki ligi mbalimbali nchini, jambo linaloonesha mafanikio ya mashindano hayo katika kukuza vipaji.
Katika mchezo wa ufunguzi wa KNK Cup 2026, uliochezwa Kata ya Uyovu, timu ya mashabiki wa Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba, na kuanza mashindano kwa kishindo.
Kwa upande wake, mkazi wa Ushirombo, Elias Patrick, alimpongeza Dkt. Doto Biteko kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya michezo, akisema mashindano hayo yamekuwa yakileta burudani, kuibua vipaji na kuwakutanisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bukombe.

Comments
Post a Comment