Na Abubakari Msita
Lyambamgongo, Bukombe – Timu ya Small Tiger imeandika historia kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Lyambamgongo baada ya kuichapa Afya FC mabao 2-1 katika fainali iliyopigwa leo kwenye Uwanja wa Kijiji cha Lyambamgongo.
Small Tiger ilianza kwa kasi baada ya Emmanuel Thomas kuifungia timu hiyo bao la kwanza dakika ya 9. Hata hivyo, Bakari Kitula aliisawazishia Afya FC dakika ya 15 na kufanya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare ya 1-1.
Mchezo uliendelea kuwa mkali huku timu zote zikitafuta bao la ushindi, lakini katika dakika ya 90, Omary Shabani aliibuka shujaa kwa kuifungia Small Tiger bao la ushindi na kuifanya timu hiyo kutwaa ubingwa wa KNK Cup 2026 ngazi ya kata.
Kwa ushindi huo, Small Tiger imejinyakulia seti moja ya jezi, mpira mpya na kitita cha shilingi 100,000, pamoja na kupata nafasi ya kuiwakilisha Kata ya Lyambamgongo katika hatua ya Tarafa. Afya FC, waliomaliza nafasi ya pili, wameondoka na zawadi ya shilingi 50,000.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Diwani wa Kata ya Lyambamgongo, Mhe. Boniphace Shitobelo, alimpongeza mdhamini wa mashindano hayo, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya michezo kupitia KNK Cup.
Alisema mashindano hayo yamekuwa daraja la kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa wananchi na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara wanaoshiriki wakati wa michezo. Pia aliwahimiza vijana kuendelea kujituma kwani michezo ni ajira na inaweza kubadilisha maisha yao.
Kwa upande wao, wachezaji walimshukuru mdhamini pamoja na waandaaji wa mashindano hayo na kuomba KNK Cup iendelee kufanyika kila mwaka ili kutoa nafasi zaidi kwa vijana kuonyesha vipaji vyao.
Comments
Post a Comment