Na, Ernest Magashi
Timu ya Shigulumule FC imeibuka bingwa wa mashindano ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Iyogelo, Tarafa ya Bukombe, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-3 kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Mataba Sugar FC kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90 za mchezo.
Mchezo huo wa fainali ulichezwa katika uwanja wa michezo Iyogelo na ulikuwa wa ushindani mkubwa huku timu zote zikionyesha kiwango kizuri. Baada ya dakika za kawaida kumalizika kwa sare ya 2-2, mwamuzi aliamuru upigaji wa mikwaju ya penalti ili kumpata bingwa wa kata.
Katika hatua hiyo, Shigulumule FC ilitumia vyema nafasi zake na kuibuka na ushindi wa penalti 4-3, hivyo kutwaa ubingwa wa Kata ya Iyogelo na kufuzu kuiwakilisha kata hiyo katika hatua inayofuata ya mashindano ngazi ya Tarafa.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Iyogelo ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mashindano hayo ngazi ya kata, Mwanjia Said, alizipongeza timu zote 18 zilizoshiriki mashindano hayo yaliyoanza Julai 1 hadi Julai 26, 2026.
Alisema mashindano hayo yamefanikiwa kwa amani na ushindani wa hali ya juu, huku yakitoa bingwa atakayewakilisha Kata ya Iyogelo katika hatua ya Tarafa. Aidha, aliwataka wadau wa michezo na wananchi kuendelea kushirikiana ili kujenga timu imara yenye uwezo wa kufanya vizuri katika hatua zinazofuata.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Iyogelo, Juma Lushiku, alipokabidhi zawadi kwa washindi kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Bukombe na mdhamini wa mashindano ya KNK Cup, Dkt. Doto Biteko, alisema mashindano hayo yameendelea kuwa chachu ya maendeleo ya michezo na mshikamano wa kijamii.
Lushiku alimpongeza Dkt. Biteko kwa kuendelea kudhamini KNK Cup kila mwaka, akisema lengo lake ni kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha umoja wa wananchi na kutoa fursa kwa wachezaji kuonekana na kukuza vipaji vyao. Aliahidi kuwa timu ya Shigulumule FC itaendelea kupata ushirikiano kadri itakavyosonga mbele kwenye mashindano.
Nahodha wa Shigulumule FC, Samuel Antony, alipokea zawadi za ubingwa kwa kumshukuru Mungu, benchi la ufundi na wachezaji wenzake kwa kujituma, akiahidi kuwa timu hiyo itapambana kwa nguvu zote ili kutwaa ubingwa wa KNK Cup ngazi ya Jimbo la Bukombe.
Naye nahodha wa Mataba Sugar FC, Bahati Emanuel, alisema wamepokea matokeo hayo kwa moyo wa michezo, licha ya maumivu ya kupoteza fainali, na kuahidi kurejea wakiwa na nguvu zaidi katika mashindano yajayo.
Mabingwa wa Kata ya Iyogelo, Shigulumule FC, wamekabidhiwa seti moja ya jezi, mpira mmoja na shilingi 100,000, huku washindi wa pili Mataba Sugar FC wakikabidhiwa shilingi 50,000 pamoja na mpira mmoja. Mashindano ya KNK Cup yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji na kuendeleza maendeleo ya soka katika Wilaya ya Bukombe.

Comments
Post a Comment