Wilaya ya Bukombe inatarajiwa kuwa kitovu cha burudani za michezo Agosti 4, 2026, ambapo Bukombe Stadium iliyopo eneo la Kilimahewa, Ushirombo Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita, itakuwa mwenyeji wa shamrashamra za kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2026/27.
Wananchi wa Bukombe na maeneo ya jirani wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia siku hiyo maalumu ya michezo na burudani, itakayoanza saa 2:30 asubuhi hadi usiku.
Akizungumza na Bukombe Sasa Media, Afisa Michezo wa Wilaya ya Bukombe, Jenipha Kisusi, alisema tukio hilo si uzinduzi rasmi wa uwanja, bali ni siku maalumu ya kuwapa wananchi fursa ya kushuhudia shamrashamra za kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu."Isitafsiriwe kuwa ni uzinduzi wa uwanja. Hii ni siku maalumu kwa wananchi wa Bukombe kujionea shamrashamra za msimu mpya wa Ligi Kuu 2026/27 na kufurahia burudani mbalimbali za michezo," alisema Kisusi.
Siku hiyo itajumuisha michezo mbalimbali pamoja na burudani kutoka kwa wasanii wadogo na wakubwa timu ya wanawake ya Bukombe itachuana na timu ya wanawake ya Geita mchezo wa kirafiki kati ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe dhidi ya wenzao wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.
Baadaye, mashabiki watashuhudia mchezo wa kirafiki utakaowakutanisha Geita Gold FC dhidi ya Pamba Jiji FC, huku viongozi wa Yanga SC wakitarajiwa kuwepo kwa ajili ya utambulisho mfupi wa kikosi pamoja na mazoezi katika Uwanja wa Bukombe Stadium.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya na Mkoa wa Geita, Domisian Kabalega, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi Agosti 4, 2026, kushuhudia burudani za michezo na kujionea kwa ukaribu ubora wa Bukombe Stadium.
Wakati huo huo, baadhi ya wadau wa michezo akiwemo Peter Shaban na Ashura Aly, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstafu , Dkt. Doto Biteko, kwa juhudi zake za kuendelea kuleta maendeleo wilayani humo, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa mpira na miradi mingine ya huduma za kijamii ambayo itaendelea kuinua sekta ya michezo na maendeleo ya wananchi.

Comments
Post a Comment