Na, Ernest Magashi
Roma FC imeibuka bingwa wa mashindano ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Bulega, Tarafa ya Kimichezo Ng'anzo-Bulenga, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, baada ya kuichapa Buseng'hwa FC kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Bulega.
Fainali hiyo ilikuwa ya ushindani mkubwa huku timu zote zikionesha kiwango cha hali ya juu mbele ya mamia ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia pambano hilo. Bao pekee la mchezo lilifungwa kipindi cha pili na mshambuliaji Daudi Zaburon dakika ya 56 na kuipa Roma FC ushindi uliowavisha taji la ubingwa wa kata pamoja na tiketi ya kuiwakilisha Bulega katika hatua ya Tarafa ya mashindano ya KNK Cup 2026.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Bulega ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mashindano hayo ngazi ya kata, Salvatory Matemu, aliwapongeza wachezaji, viongozi na mashabiki wa timu zote kwa kudumisha amani na mshikamano katika kipindi chote cha mashindano.
Alisema mafanikio ya mashindano hayo yametokana na ushirikiano mzuri wa wadau wote na kuwataka wananchi kuendelea kuiunga mkono Roma FC ambayo sasa inakwenda kuiwakilisha kata katika hatua inayofuata.
Kwa upande wake, Polisi Kata ya Bulega, Akwilini Mpeka, aliyekabidhi zawadi kwa niaba ya Diwani wa Kata ya Bulenga, Erick Kagoma, na mdhamini wa mashindano hayo, Dkt. Doto Biteko, aliwapongeza washindi na kueleza kuwa KNK Cup imeendelea kuwa chachu ya kukuza vipaji vya vijana na kuimarisha maendeleo ya michezo katika Wilaya ya Bukombe.
Nahodha wa Roma FC, Franck Erick, alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Bukombe Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kuandaa na kudhamini mashindano hayo, akisema ubingwa huo ni matokeo ya maandalizi mazuri, nidhamu na kujituma kwa wachezaji wote.
Akipokea zawadi ya ubingwa, nahodha huyo alimshukuru Mungu pamoja na wachezaji wenzake kwa kujitoa kwao, huku akiahidi kuwa Roma FC itapambana kwa nguvu zote kuhakikisha inatwaa ubingwa wa KNK Cup katika ngazi ya Tarafa na baadaye Jimbo la Bukombe.
Naye nahodha wa Buseng'hwa FC, Baraka Juma, alisema wamekubali matokeo kwa moyo wa michezo licha ya maumivu ya kupoteza fainali, akiahidi kurejea wakiwa imara zaidi katika mashindano yajayo.
Mabingwa wa Kata ya Bulega, Roma FC, walikabidhiwa seti moja ya jezi, mpira mmoja pamoja na shilingi 100,000, huku washindi wa pili Buseng'hwa FC wakizawadiwa shilingi 50,000 na mpira mmoja.
Mashindano ya KNK Cup 2026 yanaendelea kuthibitisha umuhimu wake katika kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa jamii na kukuza maendeleo ya soka katika Wilaya ya Bukombe.

Comments
Post a Comment