RANE ACADEMY YATWAA UBINGWA WA KNK CUP 2026 KATA YA UYOVU KWA KUIFUNGA RUNZEWE CITY BAO 1-0

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Timu ya Rane Academy imeibuka bingwa wa mashindano ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Uyovu baada ya kuichapa Runzewe City kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa katika Uwanja wa Uyovu, Tarafa ya Siloka, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.Fainali hiyo ilivutia mamia ya mashabiki wa soka waliojitokeza kushuhudia pambano kali lililojaa ushindani mkubwa. Bao pekee la ushindi lilifungwa na Thomas Emmanuel katika dakika ya 11, bao lililodumu hadi dakika 90 za mchezo na kuifanya Rane Academy kutwaa taji hilo.Akizungumza baada ya mchezo huo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Uyovu ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mashindano hayo, Petro Mkude, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kudhamini mashindano hayo na Diwani wa Kata ya Uyovu kwa ushirikiano alioutoa katika kuhakikisha mashindano yanafanyika kwa mafanikio.Mkude alisema KNK Cup imeanza na kumalizika kwa amani, huku timu zote zikionyesha nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja.Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Uyovu, Mathayo Kagoma, aliyemwakilisha Mbunge Dkt. Doto Biteko katika kukabidhi zawadi kwa washindi, alisema mashindano hayo tangu yalipoanza Julai 1, 2026 yameendelea kuibua vipaji vya vijana na kuimarisha mshikamano wa wananchi.Alieleza kuwa baadhi ya wachezaji tayari wameanza kuvutia timu zinazoshiriki ligi za madaraja ya juu kutokana na kiwango walichoonyesha katika KNK Cup, jambo linalodhihirisha mafanikio ya mashindano hayo.Kagoma aliwataka wachezaji wa Kata ya Uyovu kuendelea kushirikiana na kuunda kikosi imara kitakachoiwakilisha kata hiyo vizuri katika hatua ya Tarafa na baadaye ngazi ya Jimbo la Bukombe.Nahodha wa Rane Academy, Mbopa Nestory, alimshukuru Mungu pamoja na wachezaji wenzake kwa kujituma tangu kuanza kwa mashindano hadi kufanikiwa kutwaa ubingwa huo.Alisema huo ni ubingwa wa kwanza kwa Rane Academy tangu mashindano ya KNK Cup yaanzishwe mwaka 2016, na kwamba sasa wamejipanga kuwania ubingwa wa Tarafa na baadaye Jimbo la Bukombe."Tunaamini uwezo tunao. Tutaendelea kujifua kambini na kusubiri ratiba ya hatua inayofuata ili kutimiza malengo yetu ya kutwaa ubingwa wa Tarafa na Jimbo," alisema Nestory.Kwa ushindi huo, Rane Academy imejizolea seti moja ya jezi, mpira mmoja na zawadi ya shilingi 100,000, huku Runzewe City iliyomaliza nafasi ya pili ikikabidhiwa mpira mmoja na shilingi 50,000.Aidha, Diwani wa Kata ya Uyovu, Mathayo Kagoma, alitangaza zawadi ya shilingi milioni moja kwa Rane Academy kwa ajili ya maandalizi ya kushiriki hatua ya Tarafa, akieleza kuwa lengo ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri na kuwania ubingwa wa KNK Cup 2026 ngazi ya Jimbo la Bukombe.

Comments