Na, Ernest Magashiebukombesasablogspot.com.tzSerikali imegawa pembejeo za kilimo cha korosho kwa wakulima wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuiwezesha wilaya hiyo kuwa miongoni mwa maeneo yanayofanya vizuri katika uzalishaji wa korosho nchini.Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, Julai 30, 2026, wakati wa hafla ya ugawaji wa pembejeo za korosho iliyofanyika katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe na kuhudhuriwa na wakulima waliosajiliwa.
Muragili alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kukuza kilimo biashara kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kuinua kipato cha wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia zao la korosho."Tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika uzalishaji wa korosho ili Bukombe iwe miongoni mwa wilaya zinazoongoza kwa uzalishaji wa zao hili nchini. Ni muhimu kutumia pembejeo hizi ipasavyo na kwa wakati ili kupata mavuno mengi yenye ubora," alisema Muragili.
Aidha, aliwahimiza wakulima kuendelea kupanda na kutunza mikorosho, akieleza kuwa zao hilo lina manufaa makubwa kiuchumi na kimazingira, likiwemo kuchangia uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi."Korosho ni zao lenye fursa kubwa ya kiuchumi kwa wananchi wetu. Tunawahimiza wakulima kuendelea kuwekeza katika kilimo hiki ili kuongeza kipato cha kaya, kuboresha ustawi wa familia na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Wilaya ya Bukombe," alisisitiza.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Bukombe, Zedekiah Osano, alisema kilimo cha korosho wilayani humo kilianza mwaka 2023 kufuatia juhudi za Serikali za kuhamasisha kilimo biashara na kuimarisha uzalishaji wa mazao ya biashara yenye tija.Alisema hadi sasa Wilaya ya Bukombe ina wakulima 71 wa korosho, wenye jumla ya miche 15,804 iliyopandwa katika ekari 527 zilizopo katika kata nane ambazo ni Namonge, Busonzo, Butinzya, Iyambamgongo, Bulangwa, Uyovu, Runzewe Magharibi na Runzewe Mashariki.Osano alisema matarajio ya wilaya ni kuongeza idadi ya wakulima pamoja na eneo la uzalishaji wa korosho katika miaka ijayo ili kuiwezesha Bukombe kuwa miongoni mwa wilaya zinazoongoza kwa uzalishaji wa zao hilo nchini.Aliongeza kuwa kupitia Chama cha Msingi cha Ushirika wa Korosho cha Korosho Siloka AMCOS, wilaya imepokea lita 395 za pembejeo za korosho ambazo zinasambazwa kwa wakulima ili kuongeza tija na ubora wa uzalishaji.Baadhi ya wakulima walionufaika na pembejeo hizo waliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwawezesha kupitia huduma mbalimbali za kilimo, wakiahidi kuzitumia ipasavyo ili kuongeza uzalishaji, kuboresha kipato cha familia zao na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Wilaya ya Bukombe.

Comments
Post a Comment