NAMPALAHALA FC YATWAA UBINGWA WA KNK CUP 2026 KATA YA BUSONZO KWA KUIFUNGA IDOSELO WARRIORS1-0


Na,ErnestMagashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Nampalahala FC imeibuka bingwa wa mashindano ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Busonzo, Tarafa ya Siloka, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, baada ya kuichapa Idoselo Warriors kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa Julai 20, 2026 kwenye Uwanja wa Michezo Busonzo.Ushindi huo umeipa Nampalahala FC tiketi ya kuiwakilisha Kata ya Busonzo katika hatua ya Tarafa ya Siloka, ikiwa na matumaini ya kuendelea na kiwango bora ilichoonyesha tangu kuanza kwa mashindano hayo.Bao pekee la ushindi lilifungwa na Shinge Mitanga katika dakika ya 80, bao lililowafanya mashabiki wa Nampalahala FC kushangilia kwa nguvu hadi filimbi ya mwisho.Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi, Afisa Mtendaji wa Kata ya Busonzo ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa KNK Cup 2026 katika kata hiyo, Rehema Mfaume, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano hayo ambayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa jamii na kutoa burudani kwa wananchi.Kwa niaba ya mdhamini wa mashindano, Dkt. Doto Biteko, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nalusunguti Kasema Mashauri, ambaye pia alimwakilisha Diwani wa Kata ya Busonzo, aliwakabidhi zawadi mabingwa wa mashindano. Alizipongeza timu zote zilizoshiriki kwa kuonyesha ushindani wa hali ya juu na kuwataka wachezaji kuungana kuunda kikosi imara kitakachoiwakilisha Kata ya Busonzo katika hatua ya Tarafa ya Siloka.Alieleza kuwa Dkt. Biteko ameendelea kudhamini mashindano hayo kila mwaka tangu yalipoanzishwa mwaka 2016 kwa jina la Doto Cup, na sasa KNK Cup, kwa lengo la kukuza michezo, kuimarisha umoja wa wananchi na kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.Nahodha wa Nampalahala FC, Matenso Kabadi, alimshukuru Mungu pamoja na wachezaji wenzake kwa kujituma katika kila hatua ya mashindano hadi kufanikiwa kutwaa ubingwa. Alisema ushindi huo ni matokeo ya nidhamu, ushirikiano na kujituma kwa timu nzima, huku akisisitiza kuwa sasa wanaanza maandalizi ya hatua ya Tarafa ya Siloka wakilenga kufanya vizuri zaidi na kutwaa ubingwa.Kwa upande wake, nahodha wa Idoselo Warriors, Mwanyas Edwin, alisema wamepokea matokeo hayo kwa moyo wa ushindani licha ya maumivu ya kupoteza fainali. Aliongeza kuwa watajipanga upya, kurekebisha mapungufu yao na kurejea wakiwa imara zaidi katika mashindano yajayo.Bigwa amepokea seti ya jezi moja mpira mmoja na fedha shilingi 100,000 huku mshindi wa pili alipata mpira mmoja na shilingi 50,000.Huku wadau wakimuunga mkono Mdhami wa mashindano kwa kutia zawadi kwa timu nne. 

Comments